Habari Mseto

Uteuzi wa mkuu wa Lapfund wapigwa breki kufuatia madai ya zoezi kuingiliwa

February 18th, 2024 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

UTEUZI wa afisa mkuu (CEO) wa Bodi ya Hazina ya Serikali za Kaunti (LAPFUND) umepigwa breki na Mahakama kuu kufuatia madai umevurugwa kwa lengo la kumteua mtu ambaye hajahitimu.

Jaji Maureen Onyango alisitisha zoezi hilo la kumteua CEO huyo hadi pale kesi iliyoshtakiwa na chama cha kutetea wafanyakazi wa kaunti (KCGWU) isikizwe na kuamuliwa.

Kikiomba zoezi hilo lisimamishwe, Chama cha KCGWU kilimfichulia Jaji Onyango kwamba mwenyekiti wa Lapfund na CEO mwandamizi walibadilisha mwelekeo uliotolewa na bodi kuhusu kiwango cha elimu ya watakaowania wadhifa huo.

Jaji huyo alielezwa wawili hao walibadilisha agizo kwamba wanaotazamia kuteuliwa wawe wamehitimu kwa Uzamili.

Lakini wakili Peter Oginga aliyewasilisha kesi hiyo mbele ya Jaji Onyango alisema mwenyekiti na CEO mwandamizi walibadilisha kuhusu kiwango cha elimu cha watakaoomba kazi hiyo wawe na cheti cha digirii.

“Mwenyekiti wa Lapfund na CEO mwandamizi walijitwika jukumu wasilo nalo na kubadilisha mwongozo uliotolewa na bodi kuhusu kiwango cha elimu,” Bw Oginga alieleza mahakama huku akiomba zoezi hilo lisitishwe ili mtu asiyehitimu kuteuliwa kutwaa wadhifa wa CEO Lapfund.

Mahakama ilielezwa Ijumaa wiki iliyopita kwamba mwenyekiti na CEO mwandamizi walibadilisha mwelekeo uliotolewa na bodi ili CEO anayehudumu kama kinara wa hazina hiyo ya Lapfund afaulu kuteuliwa licha ya kutokuwa na digirii ya Uzamili.

Bodi hii ya Lapfund ndiyo inayodhibiti huduma zote za malipo ya uzeeni ya wafanyakazi wote wa kaunti zote 47.

Bw Oginga alieleza korti kwamba kubadilishwa kwa masharti ya elimu ya atakayeteuliwa kulifanywa kumpendelea CEO mwandamizi anayemezea mate wadhifa huo.

Mahakama iliambiwa tangazo ya wadhifa huo wa CEO Lapfund lililochapishwa katika magazeti halikuguzia kuhusu Uzamili kwa wanaotuma barua za maombi.

Jaji huyo alielezwa bodi hiyo ilipofanya kikao chake Septemba 2023 ilisisitiza CEO atakayeteuliwa awe amehitimu kwa shahada ya Uzamili.

Lakini tangazo lililochapishwa Novemba 27,2023 katika magazeti ilipuuza masharti hayo.

“Dhamira kuu ya kubadilishwa masharti ni kutafuta mbinu za kumsaidia CEO mwandamizi kupata wadhifa huo,” jaji alielezwa.

Akitoa uamuzi, Jaji Onyango alisema ombi la chama hicho cha kutetea haki za wafanyakazi wa kaunti yako na mashiko kisheria na “liko na mashiko kisheria na yapasa kukubaliwa.”

Jaji huyo alisitisha zoezi la uteuzi huo na kuamuru kesi isikizwe Machi 19, 2024.

Wakili huyo aliagizwa awakabidhi washtakiwa nakala za kesi hiyo katika muda wa siku 14.

KCGWU kimemshtaki mwenyekiti wa Lapfund, CEO mwandamizi na kampuni ya A & J Limited.

Bodi ya sasa ya Lapfund inajumuisha Mabw Roba Duba, Seth Panyako, Molu Jillo Mamo, H aro Guyo Okola, Kiricha Mwanyasi, Elyas Sheikh Abdinoor na Patrick Muiruri.

Bodi hii ilikuwa imetimuliwa Feburuari 2023 na Waziri wa Fedha Prof Njuguna Ndung’u lakini ikarudishwa na Jaji Lawrence Mugambi aliyesema kitendo cha waziri huyo kinakinzana na sheria.

Jaji Mugambi alisema kitendo cha Prof Ndung’u kilikuwa cha kufedhehesha wanachama wa bodi hiyo ya Bw Duba.

Jaji Mugambi alitimua bodi mpya iliyokuwa imeteuliwa na Prof Njuguna.

Jaji huyo alirudisha kazini bodi ya Bw Duba.

Bodi hii ndiyo iliyopitisha iteue CEO mpya.