Siasa

UTEUZI WA WANAJESHI SERIKALINI WAZUA KIWEWE

October 3rd, 2020 3 min read

BENSON MATHEKA Na KAMAU WANDERI

HATUA ya Rais Uhuru Kenyatta kukabidhi wanajeshi usimamizi wa idara na mashirika ya kiraia imezua hofu ya kuchochea utawala wa kidikteta nchini.

Lakini kwa upande mwingine kuna wachanganuzi wanaounga mkono hatua hiyo wakisema kutumia wanajeshi kumetokana na haja ya kulainisha usimamizi wa idara za serikali wakati wasimamizi wa kiraia wanaposhindwa kutekeleza majukumu yao ifaavyo ama kuhusishwa na ufisadi.

Kufikia sasa Rais Kenyatta amewateua maafisa wa jeshi ama Idara ya Ujasusi (NIS) kusimamia mashirika kadhaa ya umma.

Kati ya maafisa hao ni Meja Jenerali Mohammed Badi wa Idara ya Huduma za Jiji la Nairobi (NMS) akisaidiwa na maafisa wengine sita wa kijeshi.

Bw Badi pia atakuwa akihudhuria vikao vya Baraza la Mawaziri ingawa hajastaafu kutoka jeshini.

Mapema mwezi jana, Rais Kenyatta aliagiza Kampuni ya Nyama ya Kenya (KMC) iwekwe chini ya usimamizi wa KDF.

Mkurugenzi wa Idara ya Ujasusi (NIS) Meja Jenerali Philip Wachira Kameru pia ni mwanajeshi.

Waliotoka NIS ni Inspekta Jenerali wa polisi Hillary Mutyambai, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) Twalib Mubarak.

Kudhoofisha utawala wa kiraia

Mkurugenzi wa Idara ya Uhamiaji Alexander Muteshi alikuwa afisa wa NIS na alichukua nafasi hiyo kutoka kwa mtangulizi wake Meja Jenerali (Mstaafu) Gordon Kihalangwa.

Wanasheria na wataalamu wa usalama wanasema mtindo huu wa kushirikisha wanajeshi katika usimamizi wa masuala ya kiraia una hatari ya kudhoofisha utawala wa kiraia. Wakili Abdikadir Mohammed, ambaye alikuwa mshauri wa Rais Kenyatta, anasema jeshi halipaswi kushirikishwa katika masuala ya kiraia.

Anaongeza kuwa kufuta mpaka kati ya huduma za kijeshi na za kiraia kunaweza pia kuhatarisha sifa za jeshi la Kenya.

Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Kenya (LSK), Nelson Havi pia anapinga kutumika kwa wanajeshi katika masuala ya raia akisema hii itawafanya kujiingiza katika siasa ambazo wanapasa kutounga mkono upande wowote.

“Jukumu kuu la KDF ni kulinda nchi. Mbona Rais anawatoa wanajeshi kutoka majukumu yao na kuwaingiza kwenye siasa? Huu ni mwelekeo unaohatarisha usalama wa nchi,” asema Bw Havi.

Alisema LSK tayari imewasilisha kesi mahakamani kupinga kushirikishwa kwa Bw Badi katika vikao vya Baraza la Mawaziri.

“Kuna uwezekano hata jeshi kupanga mapinduzi ya serikali, panapokuwa na afisa wa jeshi anayejua siri za nchi kuwaliko wakubwa wake kwenye jeshi. Ni taswira hatari kwa Bw Badi kujua baadhi ya mambo ambayo wakubwa wake hawana ufahamu,” akasema Bw Havi.

Wakili Lempaa Suyanka anatoa kauli kama hiyo, akisema kuwa Rais Kenyatta anavuruga na kuhatarisha mustakabali wa nchi kwa kisingizio cha kulainisha usimamizi.

Bw George Musamali, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya usalama, anasema kuna uwezekano Rais Kenyatta anapotoshwa na baadhi ya washauri wake.

“Kenya ni nchi inayozingatia demokrasia. Wakati Rais anapoanza kuwajumuisha wanajeshi kwenye taasisi za kiraia bila kuzingatia taratibu zifaazo, hapo ndipo mfumo wa kidikteta huanza. Tuko kwenye hatari ya Kenya kuchukua mkondo wa nchi kama Rwanda na Uganda, ambazo zimegeuka kuwa mataifa yanayoongozwa kwa mfumo wa kijeshi,” asema Bw Musamali.

Anasema mbinu hiyo pia huenda ikawa ni njama ya kuficha ukweli kuhusu sakata zinazoendelea serikalini, kwani ni mtindo wa jeshi kuendesha mipango yake kwa siri kubwa.

Anaonya kuwa pia kuna uwezekano wa maafisa wa jeshi wanaohudumu katika idara za raia kukataa kurejea kambini baada ya “kuonja utamu” wa kusimamia taasisi na idara za kiraia wanakosimamia mabilioni ya fedha.

Hata hivyo, kuna wanaohisi kuwa Rais Kenyatta anatumia jeshi kukabiliana na ufisadi na kurejesha nidhamu katika idara na mashirika ya umma.

Kulingana na Wycliffe Osambwa ambaye ni mhadhiri wa masuala ya utawala katika Chuo Kikuu cha Alupe, Rais Kenyatta hajafanya makosa kutumia wanajeshi kusimamia idara za kiraia kwa kuwa wanaongozwa na rais kama Amiri Jeshi Mkuu na ambaye pia ni raia.

“Kwa kawaida, Serikali za kidemokrasia huongozwa na raia. Lakini pia jeshi liko chini ya raia, na ndiyo sababu rais, kama kiongozi wa taifa, ndiye Amiri Mkuu. Jeshi pia limepatiwa majukumu yake yote na viongozi wa kiraia,” asema.

Bw Osambwa anaeleza kwamba nidhamu ya wanajeshi na ustadi wao katika usimamizi huenda zilifanya Rais Kenyatta kuwaamini na kuwakabidhi usimamizi wa idara za serikali katika juhudi za kukabiliana na ufisadi na usimamizi mbaya.

“Ikiwa uamuzi huo utasaidia kuvunja mitandao ya ufisadi, basi na iwe hivyo. Hata hivyo, jeshi linapaswa kutekeleza majukumu yao mapya kwa uadilifu na kikamilifu. Wakikosa kufanya hivyo, watadharauliwa na raia na kupaka tope sifa zao,” akasema Bw Osambwa.