Makala

Uthabiti wa shilingi ya Kenya watajwa kuwa 'sumu' Jumuiya

April 24th, 2019 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

UTHABITI wa Shillingi ya Kenya katika soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) umetajwa kama kiini cha wafanyabiashara wa hapa nchini kuhangaika katika ushindani.

Wabunge katika bunge la jumuia hiyo (EALA) wakiongozwa na Bw Simon Mbugua wanasema kuwa suluhu la usawa katika soko hili pana ni kuzinduliwa kwa sarafu moja ya kutumika na wote.

“Shida kubwa kwa Wakenya ni kuwa, wafanyabiashara kutoka mataifa mengine wanaingiza bidhaa zao hapa nchini na kuuza kwa bei za chini, lakini wakishabadilisha pesa hizo hadi kwa sarafu za kwao, wanajipata wameunda faida za juu,” anasema Bw Mbugua.

Kwa mfano, Shilingi ya Uganda imekuwa ikibadilishwa kwa kiwango cha Sh36 za Kenya, ile ya Tanzania ikiwa katika kiwango cha Sh22, Franc ya Rwanda ikibadilishwa kwa Sh8 na ile ya Burundi kwa Sh17.

“Ukiangalia mtindo huu, utapata kuwa wafanyabiashara kutoka mataifa hayo wataingiza bidhaa zao hapa nchini kwa kuwa kuna maelewano ya soko huru, wauze kwa bei za chini ikilinganishwa na ushindani wa Wakenya, lakini wakiishia kwa benki na wabadilishe pesa hizo hadi kwa sarafu za kwao, wanawaacha Wakenya hoi kifaida,” anasema Bw Mbugua.

Anasema kuwa Wakenya wengi wanaachwa wakiwa wamepokonywa nafasi ya kushiriki biashara huru iliyo na usawa, uchumi unapokonywa sarafu za kigeni kwa kuwa wafanyabiashara hao hurejea makwao wakiwa na hela zilizobadilishwa hadi za mataifa yao na hatimaye bidhaa za Kenya zinabakia bila uteja kwa kuwa ni za bei za juu.

Anasema kuwa taifa la Kenya limekuwa na mazoea ya kukumbatia maelewano hayo ya biashara huru lakini bila kuzingatia athari zile  zinazoandamana na kulegeza masharti ya sarafu.

Rais Uhuru Kenyatta amekuwa akiteta kuwa wale maafisa wa Kenya ambao wanafaa kuwakinga wafanyabiashara wa Kenya dhidi ya miskumo hii wamekuwa wabutu kiasi cha kutelekeza uchumi wa taifa.

“Si hawa maafisa waelewe kuwa kuna njia nyingi za kuua paka… Unaweza ukasema kuwa bidhaa hizi hazijaafikia vigezo na unazifungia nje au unaweka masharti ya juu kuliko yale yanayotekelezewa bidhaa asili,” Rais amewahi kunukuliwa akiteta.

Kumekuwa na tetesi nyingi kuwa Wakenya wamegeuzwa kuwa washindani wa wenzao wa Afrika Mashariki katika soko la hapa nchini lakini likiwa halina usawa wowote kwa kiwango kikuu uhasi ukiwa dhidi ya Wakenya.

Jaa la taka

Ni katika hali hiyo ambapo kuna wadadisi ambao wanashikilia kuwa Kenya imegeuzwa kuwa kama pipa la taka ambapo linapokezwa kila aina ya bidhaa kutoka kila pembe ya Jumuia lakini bidhaa zake zikiwa  bado zinatekelezewa masharti katika mataifa hayo.

Mbunge wa Mathira, Rigathi Gachagua anasema kuwa ndio sababu amewasilisha mswada bungeni wa kuzima biashara ambayo  haina usawa katika soko hili la Jumuia ya Afrika Mashariki.

“Tunataka kuwe na utaratibu wa kibiashara. Ukiwa na mayai ya kuuza hapa nchini, unafaa utengewe eneo ambalo halina uzalishaji wa bidhaa hiyo. Na wafanyabiashara wa Kenya nao watengewe bidhaa za kuuza kwa soko za wengine. Kuwe na mikakati za kupiga jeki uzalishaji ili kusiwe na udhaifu kwamba Wakenya wanaweka bei zao juu kwa kuwa gharama za uzalishaji ziliwasinya nao wale washindani wakiwa katika hali ya kuwa na uhuru wa kuteremsha bei kwa kuwa serikali zao ziliwapiga jeki,” anasema Rigathi.