Michezo

Uthiru Vision yalenga kufuzu kwa daraja ya pili

December 11th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU za michezo mbali mbali huanzishwa kwa malengo tofauti ikiwamo kukuza talanta za chipukizi angalau wakomae na kuibuka kati ya wachezaji wa kimataifa miaka ijayo.

Taifa hili limefurika timu nyingi tu za wanaume na wanawake katika kila kona ambazo zimejitwika jukumu la kupalilia vipaji vya wahusika huku wakidhamiria kutinga hadhi ya kutumia talanta zao kujikimu kimaisha miaka ijayo.

Ligi Kuu ya KPL

Uthiru Vision FC ni kati ya vikosi 22 vinavyoshiriki kampeni za kufukuzia ubingwa wa taji la Nairobi West Regional League (NWRL) muhula huu.

”Tumepania kujikaza mithili ya mchwa kwenye jitihada za kupigania tiketi ya kufuzu kupandishwa daraja kushiriki kipute cha Ligi ya Taifa Daraja la Pili msimu ujao,” kocha wake, Philip Odhiambo anasema na kuongeza kuwa wanafahamu shughuli hazitakuwa rahisi kwani timu zote zimejipanga kiana kupigania ubingwa huo.

Aidha kocha huyo anasema katika mpango mzima wanalenga kufuzu kupandishwa ngazi kushiriki kampeni za Ligi Kuu ya KPL miaka ijayo.

Uthiru Vision ni kati ya vikosi vinavyoshiriki kipute hicho kwa mara ya kwanza baada ya kupandishwa ngazi muhula uliyopita. Kikosi hicho kilitwaa tiketi ya kupandishwa daraja baada ya kumaliza katika nafasi ya pili kwenye kampeni za Ligi ya Kaunti msimu uliyopita.

Timu ya Kemri inayoshiriki kipute hicho. Picha/ John Kimwere

Hata hivyo, kikosi hicho kimetua katika nafasi ya 11 kwa kuzoa alama nne baada ya kushinda mchezo mmoja na kutoka nguvu sawa mara moja.

Kocha huyo anadokeza kuwa bado hawajafahamu timu kali maana bado ndiyo wanaposhiriki mechi za mkumbo wa kwanza.

Anasema licha ya kampeni hizo kuonyesha huenda zikashuhudia ushindani mkali kwa upande wao wameandaa wachezaji wao imara kukabili wapinzani wao kadiri wawezavyo wakiwinda alama tatu muhimu katika kila mechi.

Pandashuka

Kocha huyo anasema ukosefu wa ufadhili ndio tatizo linalowapa wakati mgumu kwenye mipango yao kufanya vizuri msimu huu.

Timu hii hufanya mazoezi yao katika Uwanja wa Ahiti, Dagoretti Kusini. ”Ili kuchanga fedha za kutusaidia kugharamia mahitaji ya kushiriki mechi za ugenini kuna kamati ya wanachama 14 ambapo hutulazimu kuingia mifukoni mwetu,” kocha huyo alisema.

Aidha hupata huwa vigumu kwao kupata vifaa vya kuchezea ikiwamo jezi na mipira.

Uthiru Vision ilianzisha mwaka 2007 na marehemu Cosmus Muchiri kwenye juhudi za kukuza talanta za wachezaji chipukizi katika eneo la Dagoretti Kusini.

Uthiru Vision FC inajumuisha: Kelvin Kinyanjui (nahodha), David Beckham, Kinuthia Bernard (naibu nahodha), Peter Chege, Fedinand Malimba, Delvic Mwakha, Denis Keya, Collins Alphose, Brian Ngéno, Christopher Oponyo, Joseph Mbugua, Dancun Kimathi, Samuel Kuria na Arnold Majani kati ya wengineo.