Habari Mseto

Utovu wa nidhamu chanzo cha mauti ya vijana – Viongozi

January 11th, 2020 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

UTOVU wa nidhamu na maadili mema umechangia pakubwa katika vifo vya wanarika.

Wakihutubia waombolezaji wakati wa mazishi ya vijana watano waliokufa kwenye ajali mkesha wa wa mwaka mpya eneo la Kabunyony, Eldama Ravine viongozi walilaumu utovu wa nidhamu na kujitosa kwenye anasa bila mpango kuwa chanzo cha maangamizi ya vijana wengi nchini.

Wingu la simanzi lilitanda huku waombolezaji wakishindwa kujimudu majeneza ya vijana hao yalipoingizwa katika uwanja wa kanisa la Africa Inland (AIC) Poror kwa maombi.

Wahanga wa ajali hiyo walikuwa Judy Kemboi, Jimmy Kipruto, Bramwel Kosgei, Elizabeth Ikimat na Philip Kipchirchir, mwanawe mwenyekiti wa tawi la chama cha wanariadha nchini (KAA) Bw Barnabas Kitilit.

Wote watano walifariki papo hapo katika ajali iliyotokea kwenye barabara ya Eldama Ravine-Eldoret.

Ajali hiyo ilitokea alfajiri mwendo wa saa kumi na moja unusu baada ya vijana kuburudika katika mkahawa unaojulikana Tiady mjini Eldama Ravine ambapo mamia ya watu walikusanyika kuukaribisha mwaka mpya.

Polisi na wakazi wa mji huo walikabiliwa na wakati mgumu kutoa miili ya vijana hao katika mabaki ya gari hilo aina ya Nissan Wing Road.

Viongozi waliohudhuria mazishi hayo wakiongozwa na Waziri wa Masuala ya Unyunyizaji mashamba Maji Bw Symon Chelugui walikitishwa na idadi kubwa ya vijana wanaofariki katika mazingira tata kwa sababu ya malezi mabaya.

“Ni huzuni kuu kupoteza vijana hawa wenye umri mdogo katika hali ambayo ingeepukwa.Watano hawa wangelichangia masuala mbali mbali ya Uchumi wa Nchi hii,” alisema Bw Chelugui.

Waziri huyo alitoa wito kwa makanisa na mashirika ya kikristo wawashauri vijana jinsi ya kujichukua kimaisha na kuwa waadilifu.

“Tunashuhudia vijana wengi wakiangamia katika hali ambazo zingeepukwa endapo wangelipata ushauri muwafaka,” Bw Chelungui alisisitiza.

Gavana wa Baringo Bw Stanley Kiptis alisikitishwa na uozo miongoni mwa wanarika akisema umechangiwa pakubwa na utovu wa nidhamu.

Bw Kiptis alitoa wito kwa wazazi watoe ushauri nasaa kwa watoto wao.