HabariSiasa

Utumiaji wa mihadarati haufai kuwa kosa – Sabina Chege

May 29th, 2019 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

WATUMIAJI wa dawa za kulevya hawatakuwa wakikamatwa na kufungwa jela iwapo Bunge litaidhinisha mapendekezo ya kudhibiti utumiaji wa mihadarati nchini.?

Kulingana na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Afya, Bi Sabina Chege, wazo hili limependekezwa ili kutoa mwanya wa kuwasaidia kimatibabu wale ambao wameathirika na matumizi ya dawa ambazo ni pamoja na bangi, cocaine, heroin miongoni mwa zingine.

Bi Chege alisema sheria ya sasa inawachukulia wagonjwa wa utumizi wa dawa za kulevya kama wahalifu, hali inayowafanya kuadhibiwa badala ya kusaidiwa.

Akizungumza na Taifa Leo , Bi Chege alisema sheria ya sasa inawaadhibu watumiaji dawa za kulevya na kuwaacha nje wauzaji wakiendelea na shughuli zao haramu, hali inayofanya iwe vigumu kukabiliana na tatizo la utumizi wa mihadarati nchini.

Sheria ikifanyiwa mabadiliko, akaeleza, watumizi wa mihadarati hawatakuwa wakihangaishwa kwa kukamatwa na kufungwa jela, na badala yake watapokea matibabu.

“Mengi ya matatizo ya kiakili yanatokana na utumiaji wa dawa za kulevya. Huu ni ugonjwa na unapokamata mtumiaji bangi ama dawa zingine huwa hujasaidia. Huyu ni mtu ambaye anafaa kuwa hospitalini wala sio gerezani,” akasema Bi Chege.

Alisema kuwafunga watumiaji jela pia kunafanya tatizo la utumiaji wa dawa za kulevya nchini kuwa mbaya zaidi: “Unapofunga mtumiaji bangi gerezani anageuka kuwa mtumizi wa dawa kali zaidi kama cocaine na heroin kwa sababu hawezi kuvuta bangi gerezani kwani itanuka. Inabidi ageukie zile mbaya zaidi na akiachiliwa anakuwa mtumiaji sugu na mhalifu,” akasema.

“Tunahitaji sheria ambayo itasaidia kuwaokoa wengi ambao wamekwama kwenye dawa za kulevya hasa vijana walio shule za sekondari na vyuo,” akaeleza.

Kuadhibu wagonjwa

Alisema nia kuu ya kubadilisha sheria ni kuepuka kuwaadhibu wagonjwa ambao ni waraibu wa mihadarati na badala yake kuwe na sera maalum ya kuwatibu na kuwapa ushauri nasaha ili warejelee maisha ya kawaida.

Alifafanua kwamba sheria hiyo itaweka vigezo kuhusu vipimo vya dawa ambavyo vitakubalika, na kikipita kiwango hicho itachukuliwa kuwa ni ulanguzi.

“Wale ambao watanaswa wakiwa na aina yoyote ya mihadarati kwa nia ya kuuza ndio watakaoandamwa kisheria, na tutapendekeza adhabu ya ulanguzi iwe kifungo cha maisha gerezani bila faini,” akaeleza.

Alisema sheria hiyo ikipitishwa, wale ambao ni waraibu wa dawa za kulevya hawatakuwa wakijificha ili wasikamatwe mbali watajitokeza ili kusaidiwa.

“Pia wataweza kuepuka magonjwa wanayoambukizana wanapotumia sindano kujidunga wakiwa mafichoni, kushiriki mapenzi kiholela na pia kubaguliwa na jamii,” akaeleza.

“Kwa sasa kuna mpango wa kuwapa waraibu wa mihadarati sindano? za kujidunga katika kaunti za Pwani ili kuwazima kutumia sindano moja? wakiwa wengi. Hii imesaidia kupunguza maambukizi ya magonjwa kama? Hepatitis C na Ukimwi,” akasema.

Alisema Ureno imetekeleza mpango wa kutowaadhibu watumiaji na badala yake kuwapa matibabu na imefanikiwa kwa kiwango kikubwa kupunguza idadi ya watumiaji wa dawa za kulevya pamoja na athari zake kwa jamii.

“Sasa tutaandaa uhamasisho kwa umma na tuchukue maoni yao kwa nia ya kuandaa mswada wa bunge na ukijadiliwa na upitishwe kuwa sheria, uanze kutumika kama mojawapo ya maazimio makuu ya kuafikia afya bora kwa wote nchini,” akasema Bi Chege.