Habari Mseto

Uume wa mwanamume aliyevamiwa Migori wapatikana TZ

April 18th, 2019 1 min read

NA DANIEL OGETTA

POLISI katika Kaunti ya Migori wamesema wamepata nyeti za mwanamume wa miaka 31 aliyevamiwa na uume wake kunyofolewa na watu wasiojulikana mnamo Aprili 13. Tukio hili la kushangaza lilitokea eneo la Suna Magharibi.

Mkuu wa polisi katika kaunti hiyo Bw Joseph Nthenge alieleza wanahabari kwamba uume wa Felix Otieno ulipatikana mjini Sirare, Tanzania usiku wa Jumatano baada ya kuarifiwa na wakazi.

Bw Nthenge alisema kwamba maafisa wa usalama wangali wanafutilia mmoja wa waliomvamia Felix, ambaye, baada ya kugundua kwamba anasakwa, aliamua kuuacha uume huo na kuhepa. Mhalifu huyo aliubeba uume huu ndani ya karatasi.

Kwa mujibu wa Bw Nthenge, uume huo ulipelekwa katika hospitali kuu ya Migori.  Felix naye anazidi kuuguza majeraha katika Hospitali Kuu ya Kisii ambako madaktari wanasema anazidi kuimarika kiafya.

Hapo awali, chifu wa kata ndogo ya Mukuro, alisema, mwathiriwa alopovamiwa, alikuwa pamoja na rafiki yake ambaye aliponyoka na kukwepa unyama huo.

Inasemakana, Felix alidungwa mara kadhaa kabla ya nyeti kunyofolewa na wahalifu wasiojulikana na kutoweka nazo.