Habari za Kitaifa

Uvamizi mpya wa Al-Shabaab Milihoi wafufua kumbukumbu ya Katibu wa Wizara aliyetekwa

April 11th, 2024 3 min read

NA KALUME KAZUNGU

MILIHOI ni miongoni mwa maeneo ambayo yalikuwa yameanza kujenga sifa nzuri siku za hivi karibuni baada ya miaka mingi ya kupakwa tope na magaidi wa Al-Shabaab.

Ni eneo lipatikanalo kati ya Ndeu na Koreni kwenye barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen.

Kati ya mwaka 2014 na 2018, Milihoi ilisifika, hasa kwa ubaya, kutokana na jinsi magaidi wa Al-Shabaab walivyoendeleza hulka ya kulenga eneo hilo, ambapo walishambulia watumiaji wa barabara, hivyo kuwaacha wengi wakipoteza maisha, wengine wakisalia na majeraha na makovu ya maisha ilhali mali ya mamilioni ya fedha, ikiwemo magari yakiteketezwa na wahuni hao.

Itakumbukwa kuwa mnamo 2017, Milihoi iligonga vichwa vya habari pale magaidi wa Al-Shabaab walipomteka nyara aliyekuwa katibu katika Wizara ya Nyumba, Bi Maryam El Maawy baada ya kuteketeza gari lake.

Shambulio hilo lilitekelezwa Julai 13, 2017.

Bi El Maawy aliyekuwa amejeruhiwa vibaya miguuni na kifuani kwa wakati huo, aidha aliokolewa kutoka mikononi mwa magaidi hao baaadaye kufuatia operesheni kali ya wanajeshi wa kitengo maalum cha Ulinzi Kenya (KDF).

Bi El Maawy hata hivyo alifariki miezi miwili baadaye kwenye hospitali moja nchini Afrika Kusini alikokuwa akipokea matibabu kutokana na majeraha aliyosababishiwa na Al-Shabaab kwenye tukio hilo la uvamizi.

Msafara wa El Maawy

Ikumbukwe kuwa wakati wa shambulio hilo la msafara wa Bi El Maawy, mpwa wake, Bw Ariff Kassim, 21, na walinzi watano wa katibu huyo, wote waliuawa.

Ni kutokana na tukio hilo ambapo serikali imekuwa ikijizatiti kuzika historia hiyo chafu ya Milihoi kwenye kaburi la sahau.

Mnamo 2018, serikali kuu iliweka kambi ya walinda usalama kwenye sehemu mojawapo ya Milihoi kama njia mojawapo ya kusitisha utovu wa usalama uliosababishwa na Al-Shabaab.

Serikali pia iliongeza doria za polisi na KDF eneo hilo, hali ambayo iliishia kukomesha kabisa matukio ya kigaidi yaliyokuwa yakishuhudiwa Milihoi.

Kujengwa kwa na kutiwa lami kwa barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen pia kulisaidia pakubwa kuboresha hadhi ya Milihoi.

Kwa karibu miaka sita sasa, eneo la Milihoi halijashuhudia tukio au mauaji yoyote ya Al-Shabaab.

Yaani eneo hilo lilikuwa limegeuka kuwa tulivu na pendwa.

Ili kuwapa au kuwafanya watumiaji wa barabara ya Lamu-Witu-Garsen, hasa wanapofika Milihoi, kujenga imani zaidi, serikali ilifyeka vichaka na magugu yote kando kando ya barabara, hivyo kuwawezesha wapita njia kuona mbali na kujihadhari wanapomuona adui.

Aidha, shambulio la Jumanne lililoacha mtu mmoja amekufa na wawili kujeruhiwa Milihoi limewafanya wengi kukeketwa maini kwani tukio hilo limezua kumbukumbu mbaya kulihusu eneo hilo.

Wakati wa shambulio hilo, magaidi zaidi ya 20 waliojihami kwa silaha hatari walivamia magari barabarani na kuyafyatulia risasi kabla ya kuyachoma.

Magari mawili yateketezwa

Mojawapo ya magari yaliyochomwa kwenye shambulio la Al-Shabaab eneo la Milihoi kwenye barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen mnamo Jumanne, Aprili 9, 2024. Shambulio hilo liliacha mtu mmoja akifariki na wawili wakijeruhiwa. Picha|Kalume Kazungu

Jumla ya magari mawili yaliteketezwa ilhali watu wawili wakiokolewa wakiwa na majeraha madogo madogo.

“Kumekuwa na shambulio la kigaidi Milihoi. Mtu mmoja ameuawa ilhali wawili wakijeruhiwa. Wametibiwa kwenye hospitali ya Mpeketoni na tayari wameruhusiwa kwenda nyumbani. Magari mawili pia yalichowa wakati wa uvamizi huo. Maafisa wetu wako macho na msako unaendelea kuwanasa magaidi Milihoi na viunga vyake,” akasema Naibu Kamishna wa Lamu Magharibi, Bw Gabriel Kioni.

Baadhi ya waliohojiwa na Taifa Leo walieleza kutamaushwa kwao na jinsi Al-Shabaab wanavyoharibu sifa nzuri ya Milihoi ambayo ilikuwa imechukua muda mrefu kujengwa.

“Kusema kweli uvamizi wa Jumanne umeipaka tope taswira nzuri ya Milihoi. Yamezua kumbukumbu chafu ya jinsi mamia ya watu wengine na mali yalivyoishia kuangamia mikononi mwa Al-Shabaab Milihoi miaka ya awali. Hatuna imani tena na Milihoi sasa,” akasema Bw Samuel Mwangi.

Bi Susan Mwaniki aliiomba serikali kuu kupitia idara ya usalama kuwa macho kwa kuhakikisha kuna ulinzi wa kutosha kwenye maeneo yote yapatikanayo kwenye barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen na ambayo yanatambulika kwa visa vya kujirudiarudia vya Al-Shabaab.

“Ikiwa hawa magaidi wamefaulu kupiga Milihoi na kuua mtu na kujeruhi wengine, hii inamaanisha pia sehemu zingine kama Nyongoro, Ndeu, Lango la Simba na Mambo Sasa yako hatarini. Maeneo yenyewe yalikuwa yameshuhudia utulivu wa hali ya juu lakini ni dhahiri kwamba hawa Al-Shabaab wana nia ya kuchafua taswira ya haya maeneo. Walinda usalama wawe macho,” akasema Bi Mwaniki.