Makala

Uvumbuzi wake unavyochangia kuimarisha taifa kiteknolojia

August 3rd, 2020 4 min read

Na SAMMY WAWERU

Ikiwa ndoto ya James Nyakera ya kuwekeza na kufaulu katika sekta ya ufumbuzi wa teknolojia ya kimawasiliano (ICT) itatimia, basi ni kwa muda tu atangoja kabla ya aanze kufahamika kama bwanyenye.

Nyakera anasema kuwa kubadilika kwa maisha yake hadi kuhama kiwango cha wengi cha ‘mahasla’ kutamchukua muda mfupi tu, na Mungu amjalie malengo na maombi yake.

Safari hii ya kuvuna mamilioni iwapo itafanikiwa, inatokana na uvumbuzi wake wa kipekee, katika uundaji wa mashine zitakazoimarisha sekta ya biashara, kuanzia uuzaji wa bidhaa majimaji kwa kutumia mtambo wa kupima (ATM), benki – mtambo wa kuhesabu sarafu, mitambo ya kiusalama, kengele zinazoweza kutumika shuleni, makanisani na katika vyumba vya habari. Vumbuzi hizo zikiwa chache tu kuziorodhesha.

Staa huyu anasema uvumbuzi wake unaweza kuleta msisismko mkuu sokoni kupitia mitambo ya ATM, ambapo utaondolewa gharama ya kukodisha nyumba ya kazi au ya kuajiri watu wa kuhudumu katika duka lako.

Hii ni kupitia mitambo hiyo ya mauzo na ambayo ikipakiwa na bidhaa ambazo ungetaka kuuza, iwe ni maziwa, mafuta taa, mafuta ya petrol, dizeli, bidhaa zote za majimaji hata ikiwa ni pombe ile haina povu, mtambo huu utakupa kipimo cha pesa ambazo utauweka.

“Teknolojia hii inatumia Sayansi ya kuunda programu za hela na vipimo ndani ya mtambo huo na ambapo ukishauzindua, wewe kazi yako itakuwa tu kuweka bidhaa katika hifadhi ya mtambo huo na wateja wakiingia na kuweka senti, bila kusita mtambo huu unafanya hesabu na kugawa kipimo cha kutosheleza senti ulizoweka,” asema.

Isitoshe, ikiwa ni katika shule na makanisa…hata katika vyumba vya uchapishaji habari magazetini…kila mahali ambapo hutumika kengele kama kikumbusho cha muda kuyoyoma, anasema kuwa anaweza akamwondolea binadamu kazi hiyo ya kupiga kengele.

Ni ujuzi na maarifa aliyojaaliwa katika uvumbuzi wa teknolojia, na anaendelea kuyapalilia. “Nitakachofanya ni kuunda mtambo maalum wa kiteknolojia, niiweke ratiba ya kengele kulia na ninakili sauti ya ukumbusho wa jukumu linalohitajika na iwe sasa ni rasmi kengele itakuwa ikilia muda unaohitajika,” Nyakera anaelezea.

Mtambo wa kuuza mafuta ya kupikia. Picha/ Sammy Waweru

Anasema kuwa mtambo huu wa kengele, ni ubunifu aliothibitisha kufanya kazi kupitia utafiti wake.

Nchini Kenya, hakuna shirika lolote lile la kifedha lenye mtambo wa kuhesabu sarafu, mitambo iliyoko ikiwa ni ya noti pekee. Nyakera, 27, ameibuka na mtambo wa kuhesabu senti, anaoutambua kama ‘smart money monitoring system’. “Benki na mashirika mengine ya kifedha kama vile vyama vya ushirika (Sacco), wanaweza kukumbatia mtambo huu kuimarisha utendakazi wao,” anahimiza, akisema ana uwezo kuutengeneza na kuunganisha kiteknolojia na simu ya mkono, ufahamishwe kwa njia ya arafa kiwango cha sarafu zilizotiwa au kuhesabiwa.

Lakini cha kuduwaza ni ile teknolojia ya mataa na king’ora kiusalama kutoka bongo la mtafiti huyu na mfumbuzi ambaye alihitimu kozi ya Mawasiliano na Teknolojia (IT) kutoka chuo kikuu cha Mt Kenya kilichoko Mjini Thika mwaka wa 2017.

Aidha, barobaro huyu anasema atakuundia mtambo wa kiusalama wa kuwakisha na kuzima mataa na king’ora hata ukiwa kwa umbali gani na nyumba au biashara yako. “Nitakuunganishia mtambo wa kiusalama na simu yako ya mkononi na kisha niunganishe na namba za siri katika milango, madirisha au lango kuu katika nyumba au biashara yako.

“Wakati kutatokea uvamizi, hata uwe kwa umbali gani, laini katika simu yako itakupasha habari katika kioo cha simu yako, kwa njia ya arafa. Ni matukio ya moja kwa moja. Kisha, laini hiyo itagutusha zile nambari spesheli zizindue awamu ya kupiga king’ora na pia kuwakisha na kuzima kwa awamu mataa ya kiusalama na hivyo basi kuwatimua wavamizi hao,” anafafanua.

Kulingana na Nyakera, teknolojia hii pia itaachilia miale ya stima kutoka kwa king’ora kujiunganisha na maeneo ambayo yameunganishwa na king’ora na ni ya vyuma ili kuzua mipigo ya stima hivyo basi kuweka maisha ya wavamizi hao katika hatari kuu ya kunaswa na miale hiyo kama radi.

Vumbuzi zingine za mtaalamu huyu, ni mtambo (smart farm system) unaoweza kutumika katika kilimo cha vivungulio (greenhouse), unaodhibiti kiwango cha joto na maji yanayonyunyiziwa mimea. Anasema amezindua mtambo wenye uwezo kufungua na kufunga lango, na pia kuzima mataa.

Anaiambia Taifa Leo Dijitali kwamba gharama ya utengenezaji wa mitambo hiyo inategemea ubunifu Kisayansi katika kila mashine, ikiwa kati ya Sh30,000 – 80, 000. Anasema uvumbuzi wake ukigeuka kuwa biashara, mtambo mmoja unaweza kuingiza mapato kati ya Sh50,000 – 150, 000. Picha/ Sammy Waweru

 

Si eti mambo haya yote anayafanyia katika karakana kubwa ya ufumbuzi. “Utashangaa kujua kwamba natumia chumba changu cha malazi ambacho kina upana wa futi 12 kwa 10 katika kijiji cha Kiamagoko ndani ya Kaunti ndogo ya Mathioya, Murang’a kama maabara na karakana ya ufumbuzi huu. Kwa sasa, mfadhili wangu mkuu ni mamangu mzazi na ndugu zangu na ambapo wamenisaidia kuwa nikiagiza vijisehemu vya teknolojia hizi kutoka Uchina na Korea,” anasema.

Anasema kuwa pia hupata kazi za kibarua katika taasisi kadhaa kuwawekea na kuwatunzia idara zao za kiteknolojia, lakini anakolenga ni kuwa na kiwanda chake ambacho kitakuwa kikiunda mitambo hiyo na kuuza kwa wateja.

Ubunifu wake katika sekta ya teknolojia, aliukumbatia 2016, baada ya kutafuta ajira katika kampuni na mashirika mbalimbali nchini bila mafanikio. Haijakuwa safari rahisi.

Nyakera akisifia vumbuzi zake kama zinazoweza kupunguza gharama ya matumizi katika biashara, anasema kuwa shida kuu ya taifa hili ni kwamba, kuna wavumbuzi wengi hapa nchini ambao wanaweza wakaufaa uchumi wa taifa na pia wajijenge bila kusumbua serikali “lakini hakuna mikakati ya kuwapata na kuwalea hadi wafanikishe uvumbuzi wao.”

Anasema kuwa kwa sasa serikali iko katika kila jukwaa ikisema kuwa inaunga mkono kozi za kiufundi “lakini ukiangalia sera zake, kozi hizo ni ushonaji nguo, useremala na ujenzi kwa kutumia mawe, na ambapo hata hakuna uthibiti wa viwango kwa kuwa utanipata nikiwa na uvumbuzi huu wa kipekee najumuishwa katika taasisi moja ya kijijini na walio na lengo la kujipa taaluma ya kushona nguo.”

Anaendelea kueleza kwamba, uvumbuzi ni sekta moja na ambayo haifai kujumuishwa pamoja na wanaosaka kozi kwa kuwa hakuna uwiano kamwe kati ya sekta hizo mbili.

Ukosefu wa pesa kujiimarisha, ndio kizingiti cha Nyakera, ila anasema hajachoka kumwomba Mungu amuondoe katika hali hiyo ili aweze kujiendeleza kimaisha na kuifaa nchi hii.  Picha/ Sammy Waweru

Aidha, anasema serikali kuu na pia zile za kaunti hazina ufahamu kamili wa sekta ya Kisayansi na ndiyo sababu hata vile vipawa tele ambavyo huonekana katika maonyesho ya uvumbuzi kwa wanafunzi wa shule za sekondari, vyuo vikuu na taasisi zinginezo huishia kuoza mitaani na vijijini kwa kuwa hakuna sera maalum ya kuvilea hadi viwafaidi walio navyo.

Yote tisa, kumi: Ukosefu wa fedha miongoni mwa vipaji ibuka umekuwa kikwazo na kero kuu. “Vipaji wengi nchini hawana uwezo kifedha kuonyesha umahiri wao. Ni suala linalopaswa kutiliwa maanani na serikali, na kufanya hamasisho kuwaimarisha,” anahimiza Roger Wekhomba, mtafiti.