Habari Mseto

Uvundo wa majitaka wakosesha amani wakazi wa Frere Town

August 1st, 2020 2 min read

Na MISHI GONGO

WAKAZI katika eneo la Frere Town eneobunge la Nyali, Kaunti ya Mombasa, wanahofia hali zao za kiafya kufuatia mtiririko wa majitaka katika makazi yao.

Wakazi hao wameiomba kampuni ya kusambaza maji safi ya kunywa na mabomba ya majitaka kuboresha mashimo ya kuhifadhi maji hayo ili kudhibiti mkurupuko wa maradhi.

Wakiongea na Taifa Leo hapo Ijumaa, wakazi hao walisema licha ya maji ya vyooni kutiririka hadi sehemu zao za makazi, kampuni hiyo haijafanya chochote kutatua hali hiyo.

Mkazi mmoja wa eneo hilo Bw Denis Gitonga, ambaye ni muuzaji duka alisema analazimika kuvumilia uvundo mkali unaotoka kwa maji hayo kila siku.

“Maji yanayomwagika eneo hili yanatoka vyooni. Nalazimika kuvumilia harufu mbaya kila siku,tumejaribu kulalamika lakini hakuna hatua iliyochukuliwa,” akasema.

Mwingine Bi Fatuma Osman alisema anahofia watoto wake kupata maradhi kutokana na uchafu huo.

“Nina watoto wanne wadogo na tunapokuwa tunakula nzi kutoka kwa maji hayo hugusa chakula chetu,” akasema.

Aidha alieleza kuwa analazimika kufunga madirisha na milango ili kuzuia vundo hilo kuingia ndani ya nyumba yake.

“Ninapofunga milango na madirisha nazuia hewa safi kuingia, lakini sina budi,” akasema.

Apoteza wateja

Naye Bw Peter Kamau anayeuza samaki wa kukaanga kando ya barabara hiyo alisema amepoteza wateja kufuatia hali hiyo.

“Nilikuwa nategea watu wanaotumia njia hii wanapokuwa wanatoka kazini jioni, lakini kwa sasa sina wateja japo nafunika samaki wangu. Watu wanapoona maji chafu yanatiririka karibu nami wanashindwwanashindwa kununua,” akasema.

Walisema kuwa hali hiyo imetokana na kuongezeka kwa nyumba katika eneo hilo na kufanya mashimo hayo yaliyojengwa zamani kushindwa kuhimili kuongezeka kwa uchafu.

“Mashimo yaliyoko yalilenga nyumba chache lakini kwa sasa nyumba zimeongezeka na kufanya mashimo hayo kuwa madogo. Tuliambiwa serikali ya kaunti itafanyia mashimo yaliyoko ukarabati lakini paka sasa hakuna kilichofanyika,” akasema.

Mwingine Bi Rose Juma alisema wanahofia mkurupuko wa magonjwa kama malaria na kipindupindu kutokana na maji hayo.

“Mbu wameongezeka kutokana na maji hayo yaliyotuwama. Tunahofia watoto wetu kushikwa na maradhi,” akasema.