Habari za Kitaifa

Uvundo wa pasipoti kuchelewa warudi Nyayo House

February 3rd, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

JUHUDI za Waziri wa Usalama wa Ndani, Prof Kithure Kindiki, kulainisha mchakato wa utoaji pasipoti katika Jumba la Nyayo zinaonekana kugonga mwamba, baada ya viongozi na Wakenya kulalamikia ucheleweshaji wa stakabadhi hizo muhimu.

Mnamo Oktoba mwaka uliopita, Prof Kindiki alifanya ziara kadhaa katika Idara ya Uhamiaji, kwenye jumba hilo, baada ya Wakenya kulalamikia ucheleweshaji wa utoaji wa pasipoti.

Baadhi walisema kuwa walikuwa wakiitishwa hongo na maafisa wa idara hiyo ili kutolewa stakabadhi hizo.

Wengine walilalamika kungoja hadi miezi sita au zaidi ili kupewa.

Hata hivyo, ‘uvundo’ huo wa kutowajibika unaonekana kurejea tena, baada ya Wakenya kuanza kulalamikia ucheleweshaji wa stakabadhi hizo, licha ya ahadi ya Waziri “kulainisha utendakazi katika Idara ya Uhamiaji”.

Mnamo Ijumaa, kiongozi wa chama cha Thirdway Alliance, Ekuru Aukot, alisema kuwa inasikitisha kuwa hali imerejea vile vile ilivyokuwa katika idara hiyo kabla ya serikali kutangaza mikakati ya kuilainisha.

“Hali iliyo katika Jumba la Nyayo ni ya kuvunja moyo. Ni sikitiko kwa Wakenya kucheleweshewa pasipoti zao hata baada kuzilipia. Mbona uchukue pesa ikiwa huwezi kuchapisha pasipoti hizo?” akashangaa.

Aliilaumu serikali kwa kutumia jumla ya Sh700 milioni kukarabati Ikulu ya Nairobi, ilhali Wakenya wanahangaika kwa kukosa huduma muhimu kama vile kupewa pasipoti zao.

“Mbona serikali inatumia mamilioni ya pesa kukarabati Ikulu badala ya kutumia fedha hizo kununua mashine za kuchapishia pasipoti? Mbona serikali inawarai Wakenya kuenda ng’ambo kutafuta ajira ilhali hawawezi kupata pasipoti?” akaeleza mshangao wake.

Kauli hiyo inajiri siku chache baada ya Wakenya kadhaa kudokezea Taifa Leo kuhusu changamoto ambazo wamekuwa wakipitia mikononi mwa maafisa wa Idara ya Uhamiaji, wakiwarai kuwaharakishia utoaji wa pasipoti zao.

Wengine hata wameeleza ghadhabu zao kwa kuandika jumbe kwenye mitandao ya kijamii.

“Waziri Kindiki anafaa kurejea katika Jumba la Nyayo na kulainisha hali tena. Anafaa kukita kambi huko kwa mwezi mzima ili kuhakikisha mitandao ya wafisadi inayowapunja Wakenya wanaotafuta pasipoti imemalizwa yote na wahusika kufunguliwa mashtaka. Nimekuwa nikingoja kupata pasipoti yangu tangu Septemba 2023. Ninahofia kuwa kazi niliyokuwa nimeahidiwa nchini Qatar itapotea ama kupewa mtu mwingine,” akasema Bi Fridah Katana, ambaye ni mkazi wa Kaunti ya Tana River.