Makala

UVUVI: Huenda kitoweo cha samaki nchini kikawa historia tusipochukua hatua

December 20th, 2018 3 min read

RICHARD MAOSI NA MAGDALENE WANJA

Uzalishaji wa samaki nchini ulipungua pakubwa kati ya mwaka wa 2013 na 2016 – kwa asilimia 21.3 kutoka tani 163,400 hadi tani 128,600.

Uhaba wenyewe ulishuhudiwa katika maziwa makuu na kwenye mabwawa ya wafugaji wa kibinafsi katika makazi yao.

Ingawa Kenya ni mojawapo ya mataifa duniani ambayo watu wengi ni waraibu wa kula kitoweo cha samaki, siku za usoni huenda wakalazimika kusaka mbinu mbadala ya kupata kitoweo cha kila siku ikiwa hali itaendelea kuwa hivi.

Baadhi ya wavuvi katika Ziwa Nakuru wakiendesha shughuli za uvuvi wakati wa alasiri. Picha/ Richard Maosi

Kulingana na ufichuzi uliofanywa na shirika linaloendesha mradi wa “Zero Hunger Strategic Report 2018” imebainika zaidi ya asilimia 70 ya samaki na bidhaa nyinginezo zinazotokana na viumbe hawa, zimepungua kiwango cha kuhofisha.

Maeneo yaliyo mbali zaidi na ufuo wa ziwa ndiyo yaliyoathirika mno .Wengi watafikiri samaki huzaana kwa wingi katikati ya maziwa makuu lakini hali imebadilika,wavuvi wenye tamaa walipovamia mazingira hayo miaka ya hivi karibuni bila kukoma hadi ilipobainika kuwa kizazi cha samaki kinaelekea kuangamia.

Ijapokuwa nchini ufugaji wa samaki unaendeshwa na sekta mbili ,ambazo ni mabwawa na kwenye maziwa ,imebainika kuwa ni asilimia 2 tu ya wafugaji wanaowajibika kikamilifu shughuli ya kufuga samaki kwa kufuata kanuni zinazohitajika.

Wavuvi hawa wameimarisha juhudi za kung’oa magugumaji. Picha/ Richard Maosi

La kushangaza ni kuwa ustawishaji wenyewe unatekelezwa katika katika kipande cha kidogo sana cha ardhi ya takriban hekta 1.4 milioni.Hili linabainisha kuwa bado pana haja ya kutoa elimu ya kutosha kwa umma na wakulima husika waanze kuchapukia mradi huu.

“Uvuvi huchangia asilimia 0.58 ya mapato yote nchini huku thamani ya samaki ikikisiwa kuwa milioni 22,” ripoti ilisema.

Pengo linalozidi kupanuka ni kati ya wakulima wa mimea kama vile mahindi,ngano na maharagwe wakisahau kutalii sekta ya uvuvi labda ni kutokana na desturi tofauti za ulaji wa kitoweo cha samaki kimaeneo ikiaminika Nyanza inaongoza kwa walaji wa samaki.

Siku za karibuni bei ya samaki imeongezeka zaidi ya mara dufu. Picha/Ayub Muiyuro

Kulingana na ripoti hiyo baadhi ya mambo yaliyofanya kupungua kwa kiwango cha samaki nchini ni uharibifu wa mazingira pamoja na ongezeko la idadi ya watu hasa kwenye maeneo yanayozunguka visiwa.

Shughuli ya kuvua samaki imekuwa ndio njia ya kipekee kujipatia riziki kwa wakazi wengi katika maeneo yenyewe bila ya kuwepo kwa mipaka ya kudhibiti hali.

Uharibifu wa mazingira unasababishwa na ongezeko la magugu maji kama vile hyacinth ziwa Victoria, lishe ya viboko katika ziwa Naivasha na athari ya plastiki zinazoingia majini kutokana na ongezeko la viwanda mijini.

Wavuvi katika bahari Hindi wakikatiza safari baada ya kuzuiwa na chaka la magugu maji (hyacinth) katika shughuli za uvuvi. Magugu maji yamekuwa yakiharibu neti zao. Picha/Richard Maosi

“Magugumaji yametapakaa katika ziwa Naivasha na kuangamiza idadi kubwa ya samaki wanaopatikana wakielea majini baada ya kupoteza uhai. Magugu maji huharibu nyavu za kuvua na serikali ya kaunti pamoja na ile ya kitaifa inafaa kuingilia kati haraka iwezekenavyo ili kunusuru wavuvi wanaotaabika,” mwenyekiti wa wamiliki wa mashua katika Ziwa Naivasha David Kilo alisema.

Ziwa Naivasha linaongoza katika uzalishaji wa samaki katika bonde la ufa na jambo hili sio la kufumbiwa macho hasa tukizingatia uchumi wa eneo lenyewe.

Kadri idadi ya watu inavyoendelea kua ndivyo migogoro ya kushindania raslimali kidogo zinazopatikana majini samaki wakiwa ni mojawapo wanavyoangamia taratibu.

Mtalii kutoka Nakuru Jimson Ndungu akitazama ziwa Naivasha lililopigwa marufuku kuvua samaki wakati wa mchana. Hili ni miongoni mwa maziwa makuu katika Bonde la Ufa. Picha/ Richard Maosi

Mambo mengine yanayochangia kupungua kwa idadi ya samaki ni mbinu duni za uvuvi wa samaki na mabadiliko ya hali ya anga.

Wavuvi wanaovua wakitumia neti zenye mianya kidogo wamekuwa wakivua samaki bila kubagua vitoto vinavyokua.

Isitoshe hili linaendana sawia na uvuaji kupita kiasi katika maziwa ya Victoria,Naivasha,Baringo na Jipe.

“Mabadiliko ya hali ya anga yamechangia kukauka kwa maziwa na kuongeza kiwango cha joto katika maeneo ya pwani,”ripoti ilieleza.

Uvuvi kutoka kwenye maziwa unachangia asilimia kubwa ya samaki wanaovuliwa duniani. Nchini Kenya asilimia 80 ya samaki hutoka ziwa Victoria.

Ziwa Naivasha lililopigwa marufuku kuvua wakati wa mchana. Idadi kubwa ya samaki imekuwa ikitoka hapa kwa miaka kadhaa sasa. Picha/Richard Maosi

Asilimia 10 ya samaki wanaovuliwa humu nchini husafirishwa katika mataifa ya nje,huku asilimia 90 wakitumika nchini.

Mtu mmoja hula takriban kilo 4.5 ya samaki kila mwaka na imepunguza kiwango cha protini mwilini hadi asilimia 7.6.

Uvuvi pia unaaminika kuchangia tani 27,125 mwaka wa 2015.

Samaki wanaofugwa sana nchini ni Tilapia,Catfish na Trout ambao wanachukua asilimia 75 ya uzalishaji wa samaki wote duniani.

Hii ina maana kwamba kuna hatari kubwa ya kuangamia kwa viumbe wa majini miaka kadhaa inayokuja.

“Kaunti ya Nakuru inafanya juhudi kabambe kuhakikisha magugu katika ziwa Naivasha yanaangamizwa .Magugu haya yanaweza kutumika katika viwanda vya kuzalisha umeme”mkurugenzi wa uvuvi kaunti ya Nakuru Mathew Ngila alisema.