Michezo

'Uwanja wa Baba Yara hauna hadhi ya kimataifa'

February 15th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

UWANJA wa Baba Yara, ambao umekuwa ukitumiwa kwa mechi za kimataifa za Ghana si wa hadhi ya kimataifa, tovuti ya Ghana Soccernet imenukuu kocha mkuu wa klabu ya Asante Kotoko Charles Akunnor akisema.

Timu ya taifa ya soka ya Kenya almaarufu Harambee Stars inatarajiwa kuzuru uwanja wa Baba Yara mjini Kumasi mnamo Machi 22 kumenyana na Black Stars ya Ghana katika mechi ya mwisho ya Kundi F ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) 2019.

Ni katika uwanja huu ambapo Ghana ilipepeta Ethiopia 5-0 katika mechi yake ya ufunguzi ya kuingia AFCON iliyosakatwa Juni 11 mwaka 2017. Ghana iliratibiwa kualika Sierra Leone katika mechi yake ya pili ya kundi hili uwanjani humu mnamo Oktoba mwaka 2018 kabla ya Sierra Leone kupigwa marufuku na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

Asante Kotoko pia ilibandua mabingwa wa Kenya wa Kombe la Ngao, Kariobangi Sharks uwanjani humu baada ya kuwachapa 2-1 Desemba 22, 2018.

Mnamo Februari 13, 2019, klabu ya Zesco United kutoka Zambia, ambayo imeajiri Wakenya Jesse Were, Anthony Akumu na David Owino, pia ilipoteza uwanjani humu pale ilipochapwa 2-1 katika mechi za makundi za Kombe la Mashirikisho la Bara Afrika.

Tovuti ya Ghana Soccernet inasema uwanja wa Baba Yara haujafanyiwa ukarabati wowote tangu utumike katika AFCON mwaka 2008.

“Hali ya uwanja ilizua hofu kabla ya mechi dhidi ya Zesco United, huku Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) likionya Kotoko iuimarishe ama itafute uwanja mwingine kuhamishia mechi hiyo,” tovuti hiyo imeongeza na kunukuu Akunnor akisema, “Uwanja wa Baba Yara haufikii viwango vya kimataifa. (Licha ya kufanyiwa ukarabati kibodo na kampuni ya Green Grass), bado unahitaji kuimarishwa zaidi kwa sababu pia mechi za timu za taifa husakatiwa humu.”

Kenya na Ghana zilifuzu kushiriki makala ya 32 ya AFCON, ambayo Misri itayaandaa kutoka Juni 21 hadi Julai 19, 2019. Hata hivyo, zinasalia na mechi kati yao, ambayo pia itaamua mshindi wa Kundi F. Kwa sasa, Kenya inaongoza kwa alama saba ikifuatiwa na Ghana (sita) nayo Ethiopia iliachwa na alama moja baada ya ushindi wake wa bao 1-0 dhidi ya Sierra Leone kufutiliwa mbali.

Sierra Leone iliondolewa kabisa kutoka kundi hili. Mataifa mengine ambayo yamefuzu kushiriki AFCON 2019 ni Misri, Madagascar, Tunisia, Senegal, Morocco, Nigeria, Uganda, Mali, Guinea, Algeria, Mauritania na Ivory Coast. Nafasi 10 zilizosalia zitajazwa baada ya mechi za mwisho za makundi kati ya Machi 22 na Machi 26.