Uwanja wa ndege kujengwa eneo la Gatuanyaga

Uwanja wa ndege kujengwa eneo la Gatuanyaga

Na LAWRENCE ONGARO

KAUNTI ya Kiambu inapanga kujenga uwanja wa ndege katika eneo la Gatuanyaga hivi karibuni.

Mnamo mwaka 2018 kampuni ya matunda ya mananasi ya Delmonte ilitoa ekari 635 kwa Kaunti ya Kiambu, baada ya majadiliano kati ya pande zote mbili.

Makubaliano hayo yalifanyika kati ya mkurugenzi wa kampuni ya Delmonte Bw Stergios Gikaliamoutsas na aliyekuwa gavana wakati huo, Bw Ferdinand Waititu.

Gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro alisema kaunti hiyo itatenga ekari 200 ili kujenga uwanja wa kisasa wa ndege.

“Tayari kuna mikakati inayoendelea kuona ya kwamba shamba hilo lililotolewa na Delmonte linatumiwa kwa njia inayostahili ili iweze kunufaisha wakazi wote wa Kiambu,” alisema Dkt Nyoro.

Kampuni hiyo ilitoa kipande hicho mwaka wa 2018 baada ya maelewano ya kuongeza miaka 99 zaidi ili kuendelea na biashara yao hapa nchini.

Kulingana na mpangilio uliokuwepo hapo awali muda wa kampuni hiyo wa kuendelea kufanya biashara yao ulikamilika, na kwa hivyo wakalazimika kurefusha zaidi muda wao.

Hata hivyo, Dkt Nyoro alisema kabla ya jambo lolote kutendeka ni sharti wananchi wahusishwe katika mipango yote itakayoendelea kuhusu ardhi hiyo.

“Hatutafanya mambo yetu kiholela ili kunufaisha watu wachache, la! Tutaleta kila mmoja wetu kwa meza ili tujadiliane,” alifafanua gavana huyo.

Alisema iwapo mpango wa kujenga uwanja wa ndege utafaulu bila shaka, Kaunti ya Kiambu itaorodheshwa katika ramani ya ulimwengu.

“Sisi wakazi wa Kiambu tuna bahati kubwa kupata kiasi hicho cha kipande cha ardhi na kwa hivyo ni vyema pia tuketi chini na kufanya mipango itakayotusaidia sisi wote,” alisema Dkt Nyoro.

Alisema mpango kama huo ni sharti serikali kuu kuingilia kati ili kufanikisha matakwa yanayopangwa na kaunti hiyo.

Alisema mradi huo ni muhimu sana kwa sababu kampuni nyingi zitafurika katika kaunti hiyo na kuleta biashara kwa kiwango cha juu.

Alieleza kuwa mipango zingine zinazotarajiwa kuendeshwa katika shamba hilo ni ujenzi wa hospitali kubwa, shule, kumbi za starehe, na soko.

Alizidi kueleza kuwa miradi hiyo yote itakuwa muhimu kwa sababu itanufaisha kaunti jirani kama Nairobi, Murang’a, na Machakos.

You can share this post!

AU yapanga kupunguza idadi ya wanajeshi wake Somalia

Uhuru, Ruto watakiwa waridhiane