Habari Mseto

Uwanja wa ndege sasa wageuzwa malisho ya ng'ombe

June 13th, 2018 1 min read

Na OSCAR KAKAI

UWANJA wa ndege wa Kishaunet ambao umetelekezwa kwa muda mrefu katika Kaunti ya Pokot Magharibi sasa umegeuzwa kuwa malisho ya mifugo na njia za mkato za wakazi kupitia.

Uwanja huo ambao uko kilomita saba kutoka mji wa Makutano, Kapenguria ni baadhi ya miradi hewa ya serikali katika kaunti hiyo.

Mradi huo ambao ulijengwa na wakoloni miaka ya 1950 ulikuwa ukitumika kama lango la kuelekea Kaskazini mwa Kenya. Ng’ombe na punda ndio ‘abiria’ kwa huonekana wakizurura ndani ya uwanja huo huku wakazi na waendesha bodaboda wakiufanya njia ya mkato kuelekea mijini.

Wakazi wanasema ni aibu kutelekezwa kwa uwanja huo wa ndege ambao una uwezo mkubwa kuwa kitega uchumi kwao. Alipoulizwa ikiwa kuna fedha ambazo serikali imetengea kukarabati uwanja huo, Kamishna wa kaunti hiyo Bw Apollo Okello alisema kuwa hawajapokea fedha zozote kwa ukarabati wa uwanja huo. Bw Okello alisema kuwa wameomba fedha ili waweze kukarabati uwanja huo lakini hadi wa leo hawajapokea.

Gavana wa kaunti hiyo Prof John Lonyangapuo alisema kuwa ukarabati wa uwanja huo uko kwenye manifesto yake na atafanya mazungumzo na Halmashauri ya Viwanja vya Ndege nchini ili waweze kununua shamba lingine kupanua uwanja huo.

“Tuko na ardhi ambayo imetengwa lakini haitoshi,” alisema Gavana Lonyangapuo.

Wakazi walitoa ekari kumi za ardhi kwa ujenzi wa uwanja huo wakiwa na matumaini makuu ya kunufaika lakini ndoto yao bado haijatimia

“Watu mashuhuri hutumia uwanja huu wa ndege. Tungetamani kuona ndege kubwa zikishuka kwenye uwanja huu lakini umesaulika,” alisema mkazi, Daniel Siree.

Mkazi mwingine Meshack Limasya alisema, “Ikiwa serikali itaamua kukarabati uwanja huu itainua uchumi wa kaunti. Maisha yetu yatabadilika kabisa.Hatuelewi mbona uwanja huu umetelekezwa ilihali tunahitaji maendeleo.”

“Tunaishi maisha ya uchochole sababu hatuna kazi ilhali tungeajiriwa kwenye uwanja huu,”asema Bw Limasya.