Habari Mseto

Uwaziri mkuu: Hofu Uhuru, Raila wana njama fiche

December 1st, 2019 2 min read

Na OSCAR OBONYO

PENDEKEZO la ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI) kuhusu kubuniwa kwa nafasi ya Waziri Mkuu limeibua maswali kuhusu lengo halisi la Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Bw Raila Odinga.

Hili pia limechangiwa na kuimarika kwa urafiki kati yao tangu handisheki mnamo Machi 9, 2018.

Bw Odinga anaonekana kupata mamlaka mapya, kwani baadhi ya maafisa wakuu serikalini kama mawaziri wamekuwa wakifika katika ofisi yake ya Capitol Hill kumweleza kuhusu ajenda mbalimbali za serikali.

Ingawa washirika wa karibu wa Bw Odinga wanaeleza kuwa huenda akawania urais mnamo 2022, wandani wa Bw Kenyatta hawajakuwa wakijitokeza wazi kueleza mustakabali wake kisiasa.

Hata hivyo, Bw Simon Mbugua, ambaye ni mbunge katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA) anaeleza kuwa “Rais Kenyatta ndiye atachukua nafasi hiyo.”

Mapema 2019 Bw Mbugua alianza vuguvugu maalum liitwalo “akaputin” linalompigia debe Bw Kenyatta kuchukua wadhifa huo.

Neno hilo linamrejelea Rais Vladimir Putin wa Urusi ambaye amehudumu kama Waziri Mkuu na Rais kwa awamu tofauti.

Bw Mbugua anasema kuwa mpango huo uko tayari kukamilishwa.

“Sisi kama jamii ya Agikuyu hatuna mrithi wa Rais Kenyatta kisiasa kwa wakati huu. Hali ilivyo, Rais Kenyatta anaweza tu kung’atuka uongozini baada ya kumkuza na kumlea mrithi wake. Ana miaka mitano kufanya hivyo katika serikali ijayo,” akasema Bw Mbugua.

Hata hivyo, baadhi ya wandani wa viongozi hao waliambia ‘Taifa Jumapili’ kwamba hakuna mkataba wowote uliopo kati yao kugawana mamlaka ifikapo 2022.

Ingawa wadhifa uliopendekezwa katika BBI hauna mamlaka, wadadisi wanasema hali inaweza kubadilika katika mchakato wa utekelezaji. BBI inasema waziri mkuu atakuwa mbunge na atapata mshahara wa mbunge pekee.

Aliyekuwa Naibu Mwenyekiti wa Chama cha Jubilee (JP) Bw David Murathe alishangaa kuhusu sababu za baadhi ya wanasiasa kukita mawazo yao kuhusu mwelekeo wa kisiasa wa Rais Kenyatta baada ya 2022.

Anasema kwamba Rais Kenyatta ameeleza wazi atazingatia Katiba kwa kung’atuka uongozini.

Mwenyekiti wa ODM Bw John Mbadi pia ametoa kauli kama hiyo: “Wawili hao wameeleza kuwa lengo lao si la kujifaidi binafsi bali la manufaa kwa nchi nzima. Ni hadi lini watu wataendeleza uvumi kwamba viongozi hao wanalenga kubaki mamlakani?”

Waibua hisia mseto

Wawili hao wameibua hisia mseto, kwani wameendelea kutoa matamshi ya wazi kumkaidi Naibu Rais William Ruto.

Novemba 2019 Rais Kenyatta aliwaacha wafuasi wake katika hali ya mchanganyiko, alipoeleza kimzaha kwamba hangejali kuhudumu kama Waziri Mkuu.

Alisema hayo kwenye mkutano wa viongozi wa Mlima Kenya uliofanyika katika mkahawa na Sagana Lodge, katika Kaunti ya Nyeri.

Mdahalo wa mpango Bw Kenyatta kuwa Waziri Mkuu umezua hisia mseto miongoni mwa baadhi ya viongozi hasa katika Jubilee.

Kiongozi wa Narc-Kenya Bi Martha Karua ameeleza hadharani kwamba Bw Kenyatta hapaswi kuchukua nafasi hiyo.

Wiki iliyopita, Bi Karua alisema kwamba hatua hiyo itakuwa ukiukaji wa wazi wa Katiba.

Alisema kuwa Katiba ya sasa inaeleza wakati rais anapaswa kuhudumu ili kuhakikisha kuwa hakuna kiongozi anayekaa mamlakani zaidi ya miaka kumi.