Michezo

Uweza na KNH zatamba ugenini

June 4th, 2019 1 min read

JOHN KIMWERE, MAGANA

TIMU za Uweza FC na Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) zilirejea nyumbani jijini Nairobi kwa tabasamu baada ya kila moja kutwaa ushindi wa alama tatu ugenini kwenye mechi za Kundi A Ligi ya Taifa Daraja la Pili.

Baada ya KNH ya kocha, George Makambi kudhalilisha Magana Flowers kwa mabao 6-2 kwenye mechi za mkumbo wa kwanza kwa mara nyingine iliikanyanga na kuchuna alama tatu muhimu ilipoichapa mabao 3-2.

Wanasoka wa KNH, chini ya nahodha, Ben Obiri waliteremsha mchezo safi na kufanya wenyeji wao kukosa ujanja.

KNH ilitwaa ufanisi huo na kufunga tatu bora baada ya Sibomona Siboh, Alassane Lass na Peter Njama kila mmoja kuifungia bao moja.

”Kazi nzuri lakini bado kibarua kipo maana nataka kushusha Uweza na Balaji EPZ kutoka kileleni,’ kocha wa KNH alisema.

Naye kocha Charles ‘Stam’ Kaindi aliongoza Uweza FC kugaragaza Jumbo T mabao 4-1 na kutwa uongozi wa ngarambe hiyo. ”Tunazidi kusongelea tiketi ya kupandishwa ngazi msimu ujao,” kocha huyo alisema na kuongeza kuwa hakuna kulala bali wanataka taji hilo.

Kwenye jedwali, Uweza FC iko kifua mbele kwa alama 38, mbili mbele ya Balaji EPZ. Mechi zingine, Commercial FC ilitoshana nguvu mabao 2-2 dhidi ya Zetech University nayo Thunder Bird ilitoka sare bao 1-1 na Kahawa United.