Michezo

Uweza Women wachupa kileleni

June 24th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya wasichana ya Carolina for Kibera ilituzwa alama tatu bila jasho huku Uweza Women FC ikitua kileleni mwa mechi za Nairobi West Regional League (NWRL) ilipotandika Lifting the Bar magoli 3-2 Uwanjani Mathare Depot, Nairobi.

Carolina for Kibera ilitia kapuni pointi zote muhimu baada ya wapinzani wao City Queens kuingia mitini. Uweza Women chini ya kocha, Domitila Wangui ilishuka dimbani tayari kutesa na kufanikiwa kutimiza azma yake kubeba alama zote muhimu licha ya kukabiliwa na ushindani mkali mbele ya wapinzani wao.

Licha ya mchezo huo kushuhudia msisimko wa aina yake, Cindy Aluoch aliitingia Uweza Women FC mabao mawili naye Mildred Hanisi alipiga moja safi.

”Dah! Kusema kweli kamwe hakuna timu ya kupuuza tulipata ushindi mwepesi baada ya kuonyesha kivumbi kikali na wapinzani wetu,” kocha wa Uweza Women FC alisema.

Kwenye patashika nyingine, Irene Khatiala alicheka na wavu mara moja na kubeba Kibagare Girls kunasa bao 1-0 dhidi ya Amani Queens.

Matokeo hayo yamefanya Amani Queens kushuka hatua moja baada ya kupokezwa kipigo cha pili mfululizo. Kwenye jedwali, Uweza Women FC inaongoza kwa kufikisha alama 21, moja mbele ya Kangemi Ladies.

Carolina for Kibera imekamata tatu bora kwa alama 16, mbili mbele ya Amani Queens.