Michezo

Uweza Women walenga kudhihirisha makali baada ya kupanda ngazi

June 24th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

WASICHANA wa Uweza Women wameibuka kati ya vikosi vinavyotesa kweli kweli kwenye kampeni za soka ya kufukuzia taji la Nairobi West Regional League (NWRL) msimu huu.

Uweza Women inayoshiriki kipute hicho kwa mara ya kwanza imeorodheshwa kati ya timu zinazopigania ubingwa huo kwa udi na uvumba kutafuta tikiti ya kufuzu kucheza mechi za mchujo kuwania tikiti ya kupandishwa ngazi kushiriki Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza msimu ujao.

Uweza Women inapata upinzani mkali kutoka kwa wenzao wa Kangemi Ladies na Carolina for Kibera bila kuweka katika kaburi la sahau Amani Queens.

Kocha wa Uweza Women, Domitila Wangui anasema kuwa wachezaji wake wanakondolea macho kibarua kigumu.

”Ingawa Kangemi Ladies inatisha kamwe hatuwezi kuiogopa maana soka haina heshima chochote chaweza kutokea tutakapokutana,” kocha huyo alisema na kuongeza kuwa hawana budi ila wanazidi kushiriki mazoezi makali kila siku ili kujiweka fiti kukabili ushindani wowote utakatua mbele yao.

Ili kukamilisha ratiba ya msimu huu, mwanzo wa ngoma itakwaruzana na Kangemi Ladies kwenye patashika inayotazamiwa kuteremsha ushindani wa kufa mtu.

Baadaye itachuana na City Queens, Amani Queens na mwisho kutifua vumbi dhidi ya The UoN Queens. Kocha huyo alisema kwamba wanapania kucheza kila mechi kama fainali maana patashika zote ni muhimu kwa kuzingatia wanahitaji kushinda zote ili kujiweka pazuri.

Naye kocha mkuu wake, Charles ‘Stam’ Kaindi anasema katika mpango mzima hawana la ziada mbali wanalenga kupigana mithili ya mchwa kuhakikisha wameibuka kidedea na kunasa nafasi ya kuwania tikiti ya kusonga mbele.

”Ni kweli kwamba licha ya kujiwekea tamanio la kusonga mbele tunakabaliwa na ushindani mkali mbele ya wapinzani wetu,” alisema na kuongeza kuwa wamekusudia kujikaza kisabuni hadi mchezo wa mwisho.

Kadhalika alisema kuwa hana shaka na wasichana wake maana wanazidi kuonyesha kwamba wanataka kupandishwa ngazi kushiriki kipute cha hadhi ya juu msimu ujao. Alidai kwamba ana imani na wachezaji wake watafanya vizuri kwenye mechi zilizosalia na kuwapiku wapinzani wao.

Kwenye msimamo wa michuano hiyo, Kangemi Ladies ingali kidedea kwa kuzoa alama 20, mbili mbele ya Uweza Women. Kwa kuzoa alama 16 wasichana wa Carolina for Kibera wamefunga tatu bora. Nao wanasoka wa Amani Queens ya kocha, Bernard Chweya wametua nafasi ya nne kwa kukusanya pointi 14.