Uweza Women yawapa akina dada jukwaa la matumaini kukuza talanta na kuimarisha maisha kimaadili

Uweza Women yawapa akina dada jukwaa la matumaini kukuza talanta na kuimarisha maisha kimaadili

Na PATRICK KILAVUKA

KWA kuzingatia kwamba mtoto uleavyo ndivyo akuavyo, timu ya kabumbu ya Uweza Women iliyo katika mwavuli wa Uweza Soccer Academy mtaani Kibera kaunti ndogo ya Kibra, iliazimia kulea vipaji vya kandanda kusawazisha maisha ya kijinsia na talanta kwa akina dada.

Isitoshe, jukwaa hili la kupalilia vipawa vya soka, limetoa afueni na kuyaweka matumaini ya mabinti hawa kuwa hai kwani, limewatenga na maovu mbalimbali ya kijamii na hata kuwapa fursa mbadala ya maisha. Kwa mfano; wengine wanadhaminiwa masomo na kusaidiwa kupitia ushauri nasaha hali ambayo imewaimarisha zaidi!

“Tulitambua umuhimu wa kuhusisha mtoto wa kike katika mpango mzima wa kukuza talanta na kuboresha maisha yake kwa kuamusha ari na kiu ya kukuza talanta za soka kwa sababu tuligundua kwamba, walikuwa na utajiri na tajriba ya soka ambayo ilikuwa imelala tu kiporo na sasa wanadhihirisha uwezo wao,” alikiri kocha mkuu Charles Kahindi.

Wengine wanaokubaliana na kauli hiyo ni mkufunzi Abdul Abubakhari na meneja wa timu Joakim Ongina.

Kocha mkuu Kahindi anasema ameona manufaa ya kulea wanavipawa hawa ambao wamekombolewa na wametambua umuhimu wa kujisawazisha kimaisha kwani wamekuwa na bidii ya mchwa kufanya mazoezi hali ambayo imempa moyo wa kuendelea kustahamili dhoruba za kujenga himaya ya timu kuwa zizi litakalosaidia akina dada wengi.

Isitoshe, waafikie hatima zao za kitalanta na maisha.

“Tangu tuanzishe timu hii mwaka 2008, tumeona vipawa vya ajabu vikijitokeza. Isitoshe, bidii na ari yao imetupa mshawashi kwamba, kazi tunayofanya si ya bure na timu sasa imegubia vikosi mbalimbali kujenga mnara wa timu kwa vizazi tofuati,” anasema Kahindi ambaye anaongoza kambi hii yenye wanasoka chipukizi 45 na wazima 30 wa kuanzia miaka isiozidi minane, U-11, U-13, U-15, U-17 na U -25.

Wengi wa wachezaji hawa ni wa shule za msingi na sekondari japo kunao walio vyuoni.

Sababu ya kuwa na vitengo hivyo kulingana na wadau ni kuhakisha kwamba matakwa ya kisoka yatakidhiwa na azma ya soka kuendelezwa mtaani.

Kikosi cha Uweza Women kutoka Kibera, kaunti ndogo ya Kibra kikipokea mawaidha kutoka kwa makocha na meneja wa timu wakati wa mechi ya kujipima nguvu dhidi ya Kangemi Ladies (Starlet) katika uwanja wa Shule ya Msingi ya Gatina Kawangware, kaunti ndogo ya Dagoretti Kaskazini. Picha/ Patrick Kilavuka

Mwaka huu 2021 wamesajili wachezaji wanne kutoka kitengo cha wasiozidi miaka 17 ambao wameinuka kisoka kuchezea kikosi wazima wakiwa Mercy Afandi, Marine Awour, Sharon Musangiza na Sharon Akinyi.

Kikosi cha U-25 kinashiriki Ligi ya Kaunti ya Shirikisho la Soka Kenya (FKF), Nairobi West.

Msimu ambao ulivurugwa na msambao wa 2020, waliponea chupuchupu kuingia ligi Daraja ya Kwanza Kitaifa baada ya kudondoshwa na Kangemi Ladies ambao waliongoza nao wakachukua nafasi ya pili.

Wadau wanasema msimu huu, wanajitahidi ukucha kwa jino kuhakikisha kwamba wamepanda ngazi.

Wameiweka timu katika zoezi kali ambalo huanza saa kumi hadi saa kumi mbili jioni siku ya Jumanne hadi Ijumaa na hata kujipiga jeki kwa mechi za kirafiki.

Maandalizi yao katika msimu yalipamba moto pale ambapo walianza kucheza mechi za kujipima nguvu dhidi Amani Ladies na kubwagwa 2-1 kuandikisha sare mbili za 1-1 dhidi ya Sunderland FC na Girl Soccer mtawalia kisha kutandikwa na Kangemi Ladies 3-1.

Mikakati inayolengwa sasa ni kuikuza timu kuweza kupanda msimu ujao hadi daraja ya kwanza ya kitaifa, kuchonga wachezaji ambao huduma zao zitanaswa na timu za primia na daraja nyinginezo nchini, kuwatafuatia wanaosoma ufadhili na kuwahamasisha zaidi katika maadili ili maisha yao yainuke.

Wadau wanawashukuru wazazi kwa kuiunga mkono na kuwa na jukumu la kufuatilia kile wanao wanafanya kuona kwamba wanaendelea kupata fursa itakaoinua maisha yao pasi na kutelekezwa.

You can share this post!

Manchester United wathibitisha kuwa jeraha litamkosesha...

Beki matata wa Leicester City, Wes Morgan, kustaafu soka...