Afya na Jamii

Uwezo wangu chumbani ni hafifu mno, nadhani ni shinikizo la kazi

June 11th, 2024 1 min read

Mpendwa Daktari,

Nimekuwa nikikumbwa na tatizo wakati wa kushiriki tendo la ndoa na mke wangu.

Sina nguvu na mara nyingi burudani imekuwa ikidumu kwa muda mfupi. Nashuku kwamba hali hii inatokana na shinikizo la kazi na ratiba yangu. Nifanyeje?

Clint, Nairobi


Mpendwa Clint,

Tatizo la kusimika mara kwa mara halipaswi kusababisha wasiwasi.

Hata hivyo, ikiwa litaendelea kwa muda mrefu, basi huenda ni kutokana na matatizo mengine ya kimwili na/au kimawazo kama vile mafadhaiko, wasiwasi, matatizo ya mahusiano miongoni mwa mengine.

Huenda ana tatizo la kimwili linaloathiri uwezo wako wa kusimika, kwa mfano kupungua kwa viwango vya testosterone, maradhi ya moyo, viwango vingi vya cholesterol, mishipa ya damu iliyoziba, kisukari, baadhi ya dawa za kukabiliana na shinikizo la damu, matatizo ya usingizi, unene, unywaji pombe kupindukia, matumizi ya sigara au aina ingine ya mihadarati, majeraha ya uti wa mgongo au katika sehemuya fupanyonga, kuchipuka kwa tishu ya kovu kwenye uume.

Aidha, huenda hamu yako kwa tendo la ndoa imepunguka kutokana na viwango vy a chini vya testosterone au kwa sababu ya matatizo ya kisaikolojia na mahusiano.

Tatafuta ushauri kutoka kwa mtaalamu wa mfumo wa uzazi wa kiume (Urologist) ili akusaidie kutambua tatizo na hata kukupa tiba.

Unachopaswa kufanya kwa sasa ni kudumisha lishe bora, kufanya mazoezi kila mara, pata usingizi wa kutosha (masaa 7 hadi 8 kwa siku), usinywe na pombe wala kuvuta sigara, na utafute njia za kukabiliana na msongo wa mawazo.