Habari MsetoSiasa

Uzembe wa Seneti huenda ukamnusuru Waititu

January 11th, 2020 2 min read

Na DAVID MWERE

HUENDA mchakato wa kumwondoa mamlakani Gavana wa Kiambu, Ferdind Waititu ukagonga mwamba baada ya kubainika kuwa Bunge la Seneti lilikiuka sheria kwa kutoshughulikia suala hilo ndani ya muda uliowekwa.

Kwa mujibu wa kipengele 33 (3) cha Sheria ya Serikali za Kaunti, ndani ya siku saba baada ya kupokea maamuzi ya kumtimua Gavana kutoka kwa Spika wa Bunge la Kaunti, spika wa seneti anapaswa kuitisha kikao cha Seneti kujadili madai dhidi ya gavana husika.

Mnamo Desemba 19, 2019 madiwani wa kaunti ya Kiambu walipitisha hoja ya kumng’oa mamlakani Gavana Waititu ambaye alizuiwa na mahakama kuingia afisini baada ya kushtakiwa kwa makosa ya ufisadi na matumizi mabaya ya mamlaka.

Ingawa Spika Stephen Ndichu, wa bunge la Kaunti ya Kiambu, aliwasilisha uamuzi wa madiwani hao kwa Spika wa Seneti Kenneth Lusaka mnamo Desemba 23, 2019, hadi sasa hajaitisha kikao maalumu kushughulikia suala hilo, hata ingawa maseneta walikuwa likizoni.

Kulingana na sheria, suala hilo lilipasa kushughulikiwa mwaka jana, ndani ya siku saba baada ya kuwasilishwa kwa uamuzi huo afisini mwa Bw Lusaka. Seneti imewahi kuzingatia utaratibu huo awali kuhusiana na kesi sawa na hii iliyomkabiliwa Bw Waititu.

Baada ya kukabiliwa na lawama za kuchelewesha suala hilo, Bw Lusaka sasa anasema ataitisha kikao maalum cha seneti Januari 21 kujadili hoja ya kuondolewa afisini kwa Gavana Waititu.

“Kiongozi wa wengi Kipchumba Murkomen amependekeza kikao maalum kufanyika Januari 21, 2020. Anakusanya sahihi za maseneta ili kufanikisha mpango huo,” Bw Lusaka akasema.

Kwa sababu muda wa kushughulikiwa kwa suala hilo umepita, kikao chochote kitakachoitishwa na Seneti kulishughulikia huenda kikapingwa kortini na hivyo kumwezesha Gavana Waititu kuponyoka.

Katika hali hiyo, madiwani wa Bunge la Kaunti ya Kiambu watalazimika kuwasilisha upya hoja ya kumwondoa mamlakani Bw Waititu, hatua ambayo itagharimu pesa za umma, kwa misingi ya Seneti kufeli kufanya kazi yake.

Kulingana na Wakili Mutakha Kangu, Spika Lusaka ndiye alifeli kutekeleza wajibu wake wa kuitisha kikao maalum. “Bw Lusaka aliamua kukiuka sheria kimakusudi, hali ambayo inafedhehesha na kuonyesha kuwa huenda ameingiza siasa katika suala hilo,” akasema mtaalamu huyo ambaye aliongoza jopo kazi lililobuni sheria zinazoongoza serikali za kaunti.