VALENTINE OBARA: Juhudi za kuzima uhalifu zisiwe ‘kiini macho’ tena

VALENTINE OBARA: Juhudi za kuzima uhalifu zisiwe ‘kiini macho’ tena

NA VALENTINE OBARA

WAKATI wowote uhalifu unapoongezeka katika maeneo ya Pwani, wadau wa usalama huanza kuwatia moyo wananchi kuhusu mikakati inayowekwa kukabiliana na magenge ya uhalifu.

Hivi majuzi, maafisa wakuu wa usalama Pwani walijitokeza kutangaza kuwa kikosi kipya kitaletwa kuangamiza magenge hayo ya vijana ambao wamekuwa wakihangaisha wakazi mchana na usiku mitaani.

Tangazo hilo bila shaka ni la kutia moyo kwa kuwa wananchi wanataka uhuru wa kuishi na kuendeleza shughuli zao muhimu wakati wowote bila kutishiwa maisha.

Inatia moyo pia kuona jinsi polisi walivyoanza kuzidisha upigaji doria katika baadhi ya mitaa ambayo imekuwa sugu kwa uhalifu kwa miaka mingi hasa katika Kaunti ya Mombasa.

Hata hivyo, suala hili la ukosefu wa usalama linahitaji kuchukuliwa kwa uzito unaostahili na litafutiwe suluhisho la kudumu. Magenge hayo ya vijana huwa hayana maarifa kwani mbinu zao ni zilezile za jadi, na haieleweki kwa nini polisi wetu walio na tajriba ya hali ya juu bado wanakosa kuyazima.

Baadhi ya maafisa wa usalama husema wanaamini magenge hayo ya uhalifu hufadhiliwa na wanasiasa na walanguzi wa mihadarati ambao wanadhamiria kutimiza maslahi yao ya kibinafsi.

Kwa wanasiasa, magenge ya vijana husemekana kutumiwa hasa katika kipindi cha uchaguzi mkuu ili watishie wapigakura wanaoaminika kuegemea pande pinzani.

Makundi hayo ya vijana ambao wengine wana umri wa chini ya miaka 15, husemekana pia kutumiwa na walanguzi wa mihadarati kupigana vita dhidi ya makundi ya walanguzi wanaoshindana nao, na katika harakati hiyo ndipo raia pia hupatikana na kuathiriwa.

Vilevile, wengine wao hujitosa katika uhalifu ili kujitafutia mapeni ya kukata kiu ya dawa za kulevya kila siku. Licha ya mambo hayo yote kusemwa na baadhi ya maafisa wa polisi, hatujaona hatua kubwa zikichukuliwa kujaribu kuwanasa wanasiasa na walanguzi wa dawa za kulevya wanaosemekana kufadhili vijana hao.

Ikiwa kweli kuna watu wanaojificha nyuma ya vijana kuhangaisha jamii, jambo la busara ni kuwafuata, wakamatwe na waadhibiwe ipasavyo.

Hiyo ndiyo njia mwafaka ambayo itasaidia kupunguza au hata kukomesha kabisa matukio ya mara kwa mara ambapo raia wasio na hatia hushambuliwa mitaani.

Mbali na hayo, masuala yanayofanya iwe rahisi kwa watoto wavulana na vijana kuingizwa katika makundi ya uhalifu pia yatazamwe kwa makini.

Mengi yametajwa kuhusiana hasa na hali ya ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana lakini kwa mtazamo wangu, kuna mambo zaidi ambayo yanafaa kuzingatiwa katika jamii.

Ikiwa kweli magenge yanatokana na ukosefu wa ajira, tujiulize kwa nini watoto wanaofaa wawe shuleni pia wamo katika makundi hayo. Hii inaashiria kuna tatizo kubwa katika jamii ambalo wadau wote wanaoshughulikia masuala ya watoto wanafaa kuchunguza kwa makini.

Kama tatizo liko katika mbinu za ulezi, mikakati itafutwe kusuluhisha hilo hata kama itabidi kuwaadhibu wazazi wanaozembea kulea watoto wao inavyotakikana.

Juhudi ziwekwe pia kuwahimiza na kuwatia moyo watoto kuhusu hali yao ya maisha ya baadaye. Hii ni kutokana na kuwa, kuna uwezekano wengi wao hawaoni maana ya kutilia maanani elimu.

Ni vigumu kuwaonyesha watoto njia mwafaka ikiwa vielelezo katika jamii ni majambazi, mafisadi, wauaji, makahaba, walanguzi wa dawa za kulevya na watumiaji wa mihadarati kupindukia.

  • Tags

You can share this post!

Kalonzo aonekena kujaa masumbuko

KINYUA BIN KING’ORI: Wawaniaji wenza sasa...

T L