VALENTINE OBARA: Magavana wajitolee kugawia manaibu majukumu ya hakika

VALENTINE OBARA: Magavana wajitolee kugawia manaibu majukumu ya hakika

NA VALENTINE OBARA

KWA muda mrefu tangu serikali za ugatuzi zianzishwe chini ya Katiba ya sasa mwaka 2013, kulishuhudiwa mizozo baina ya magavana na manaibu wao katika kaunti mbalimbali.

Hali hii ilitatiza utoaji huduma kwa umma kwani muda mwingi ulipotelea katika mizozo, huku maafisa wa kaunti na madiwani wakigawanyika kati ya walio waaminifu kwa gavana na wale waaminifu kwa naibu wake.

Kadri miaka ilivyosonga, baadhi ya magavana waliona mwanga na kuamua kudumisha uhusiano mwema na manaibu wao.

Mwaka huu, kaunti za Mombasa na Kilifi ni miongoni mwa zile ambazo magavana wametangaza wazi majukumu ya manaibu.

Punde baada ya kuingia mamlakani, Gavana Abdulswamad Nassir alitangaza kumkabidhi naibu wake, Bw Francis Thoya, majukumu ikiwemo kusafisha jiji hilo.

Kwa upande wake, Gavana wa Kilifi, Bw Gideon Mung’aro, alitaja majukumu ya naibu wake ikiwa ni pamoja na kutafuta ushirikiano wa kimaendeleo nje.

Mombasa ilikuwa inazama kwa taka zilizozagaa mitaani ikiwemo katikati mwa jiji.

Licha ya taka hizo kulaumiwa kwa kusambaza maradhi hasa ya bakteria, utawala uliokuwepo haukuonekana kujali.

Kwa sasa, wiki chache baada ya uongozi mpya kushika usukani, wakazi wameona afueni. Serikali ya kaunti imetia bidii kuzoa takataka na kuweka mtindo mpya wa kuhakikisha majaa haramu hayarudi tena mitaani.

Matarajio ya wengi ni kuwa, mtindo huu utadumishwa wakati wote kwani tumeshuhudia serikali mpya zikianza kazi kwa pupa kisha baadaye zikaanza uzembe.

Hatua ya Bw Nassir na Bw Mung’aro kuwapa majukumu manaibu wao ni jambo la kuigwa na magavana wengine wote.

Hakuna haja kumweka naibu gavana afisini, awe akila mshahara na marupurupu ilhali hakuna kazi zozote za maana anafanya.

Kiongozi bora ni yule ambaye ana uwezo wa kutambua umuhimu wa kugawa mamlaka kwa walio chini yake, wakati wowote inapohitajika.

Hatua hii itasaidia kuwezesha utoaji huduma kwa njia bora, kwani kila afisa aliyeajiriwa ana maono na uwezo ambao ukitumiwa vyema, utatoa mchango mkubwa katika kutekeleza ajenda za utawala ulio mamlakani.

Hii ni tofauti na kiongozi anayetaka kudhibiti mamlaka yote, pengine akihofia wadogo wake watapata sifa kumliko wakionekana wakichapa kazi ipasavyo.

Itakuwa bora iwapo katika miaka ya usoni magavana wote nchini wakiweka wazi majukumu yatakayotekelezwa na manaibu wao, mbali na majukumu ya mawaziri, maafisa wa idara za kaunti na wengine wanaohudumu katika afisi ya gavana.

Kwa kufanya hivi, wananchi na wadau wengine wanaofuatilia masuala ya uongozi watapata fursa bora ya kujifanyia utathmini ili kujua kama kodi na ushuru zinazotumiwa kwa mishahara na marupurupu ya watumishi katika serikali za kaunti, zinawaletea manufaa yoyote au watumishi wanalipwa bure.

  • Tags

You can share this post!

Ingwe wataka Namwamba afufue soka kuanzia mashinani

KINYUA BIN KING’ORI: Viongozi wa eneo la Nyanza...

T L