VALENTINE OBARA: MCAs waelezee wanayokamia kufanyia raia wakichaguliwa

VALENTINE OBARA: MCAs waelezee wanayokamia kufanyia raia wakichaguliwa

NA VALENTINE OBARA

IDADI kubwa ya wapigakura wanapoendeleza mijadala kuhusu Uchaguzi Mkuu unaopangiwa kufanyika Agosti 9, macho mengi yameelekezwa kwa nyadhifa kuu kama vile urais na ugavana.

Katika kaunti za maeneo ya Pwani, tumeshuhudia namna viti hivyo viwili, mbali na ubunge vimevutia sana midahalo kuhusu uwezo wa huyu au yule kutekeleza hiki na kile kwa wakazi.

Ahadi nyingi zimetolewa kufikia sasa, kila mwaniaji kiti akijisawiri mbele ya wapiga kura kwamba, ana uwezo wa kuwaondolea taabu ambazo zimewakumba kwa miaka na mikaka.

Hata hivyo, hali hii nzima inafanya wengi kutotilia maanani mojawapo ya viti muhimu zaidi katika utawala wa ugatuzi, ambacho ni udiwani almaarufu MCA.

Tangu nchi hii ilipoanza kutekeleza mfumo wa uongozi wa ugatuzi mnamo 2013, kiti cha udiwani hakijachukuliwa kwa uzito unaostahili kwa uongozi wa kaunti.

Katika utawala wa kaunti zetu, madiwani ndio wana mamlaka ya kupitisha sera na sheria zinazoongoza utekelezaji wa shughuli karibu zote za serikali za kaunti.Hivi sasa, kaunti nyingi za Pwani zinakumbana na changamoto ambazo zingeshatatuliwa ndani ya miaka kumi iliyopita ya ugatuzi. Ni changamoto hizo hizo ambazo wanasiasa wanaowania viti vya urais, ugavana na ubunge wamerudi kuahidi kuzitekeleza, huku ahadi za wagombeaji wengi wa udiwani zikihusu tu masuala mengine madogo madogo.

Mabunge ya kaunti yanastahili kuwa na madiwani ambao wamejitolea kutetea haki za wananchi dhidi ya maafisa wa afisi za magavana ambao hawana nia za kurekebisha hali ya maisha ya wakazi wa maeneo yao.

Matatizo yanayoandama Wapwani na wageni wa ukanda huu kama vile uchafu mitaani, ukosefu wa maji safi ya kwa matumizi ya nyumbani, mazingira magumu ya kufanyia biashara na kodi za juu zinazofurusha wawekezaji, ukosefu wa uwekezaji katika sekta za kilimo katika kaunti zilizo na rotuba za kutosha, miongoni mwa mengine ni mambo ambayo mabunge ya kaunti hayafai kukubaliwa kukwepa lawama.

Katika baadhi ya kaunti zetu, mabunge ya kaunti yamegeuka tu kuwa kumbi za kupitisha mapendekezo yoyote yale yanayotolewa na afisi ya gavana, bila kujali athari za mapendekezo hayo kwa maisha ya wananchi.

Ugavi wa fedha hufanywa kwa njia za kutiliwa shaka ambapo baadhi ya sekta muhimu zinazogusia moja kwa moja maisha ya raia, hazijakuwa zikitiliwa maanani kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita. Wawaniaji udiwani wanapoingia mitaani kujipigia debe, waeleze wazi iwapo wanafahamu majukumu wanayofaa kutekeleza, na mikakati waliyoweka kuwaongoza kufanikisha majukumu hayo.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Serikali ichunguze wanachofanya waliopewa leseni...

Munya ahimiza wakulima wakumbatie teknolojia za kisasa

T L