VALENTINE OBARA: MCAs wafanye hima kuwapa Wapwani matunda ya ugatuzi

VALENTINE OBARA: MCAs wafanye hima kuwapa Wapwani matunda ya ugatuzi

Kwa mujibu wa Katiba na sheria nyingine zinazohusu masuala ya utekelezaji wa ugatuzi, mabunge ya kaunti yana majukumu makubwa mno katika kutimiza malengo ya serikali za kaunti.

Ni katika mabunge haya ambapo sheria za kaunti hubuniwa na kupitishwa, na pia ni hapa ambapo madiwani wanafaa kufuatilia kwa karibu mienendo ya viongozi wakuu wa kaunti.

Mwaka huu taifa linaingia katika awamu nyingine ya ugatuzi. Kuna baadhi ya kaunti ambapo magavana walioondoka walikuwa wameongoza kwa vipindi viwili vinavyokubalika kisheria.

Kaunti za Pwani zinaanza awamu mpya ya uongozi kukiwa bado na changamoto nyingi za tangu jadi, ambazo hazijatatuliwa kwa miaka kumi iliyopita.

Hii ni licha ya kuwa, matumaini ya wengi wakati Katiba iliyoleta ugatuzi ilipitishwa 2010, ni changamoto hizi sugu zingepewa kipaumbele na kutatuliwa haraka.

Miongoni mwazo ni kama vile ukosefu wa maji safi ya mifereji mitaani, ada za juu za kufanya biashara, huduma duni za uzoaji taka, ukosefu wa mbinu bora za kusafirisha majitaka na utoaji huduma hafifu za afya ya umma.

Haya ni baadhi ya mambo ambayo sharti mabunge ya kaunti yatilie maanani, wakati huu madiwani wanajiandaa kuanza kazi.

Itasikitisha sana iwapo tutaona ajenda kuu za kwanza zikihusu masuala yanayonufaisha madiwani wenyewe au wakuu wa kaunti; kama vile kuongeza mishahara na marupurupu au kutengewa fedha za anasa ikiwemo safari za kifahari zisizo na maana yoyote kimaendeleo.

Idadi kubwa ya madiwani waliotangulia walitemwa debeni kwa sababu walishindwa kutimiza matamanio ya wananchi.

Walio mamlakani sasa wajue walichaguliwa kufanyia kazi wananchi wala si kutumia mamlaka kujitafutia makuu.

Vilevile, wasikubali kamwe kuwa vibaraka wa magavana wala wakuu wengine wa kaunti kwa kupitisha hoja ambazo zitakuwa dhalimu kwa wananchi.

Kuna mabunge yatarajiwa kuwe na mivutano kati ya madiwani wa vyama tofauti, na hili litaathiri utoaji huduma kwa umma.

Japo wawakilishi wadi hao watatoka vyama tofauti na kile cha gavana, wasiwe wepesi kupinga kila jambo linalowasilishwa kwao.

Watie kila hoja kwenye mizani na kupitisha zitakazoimarisha maisha ya wananchi.

Muhimu zaidi, ushirikiano udumu kati ya asasi zote zinazohusika katika usimamizi wa kaunti zetu ili raia wafurahie matunda ya ugatuzi yaliyochelewa.

  • Tags

You can share this post!

Tenisi ya Ferdinand Omanyala yavutia chipukizi 120

Raila ashuka bei ngomeni mwake

T L