VALENTINE OBARA: Mchakato wa kumchagua gavana Mombasa umegeuka jinamizi kuu

VALENTINE OBARA: Mchakato wa kumchagua gavana Mombasa umegeuka jinamizi kuu

NA VALENTINE OBARA

KATIKA kipindi chote cha Uchaguzi Mkuu, hakuna kaunti ambapo wakazi wamepitia mkanganyiko usio na kifani kuchagua gavana mpya kuliko Mombasa.

Mkanganyiko wenyewe ulizidishwa dakika za mwisho wiki hii wakati Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Bw Wafula Chebukati, alitangaza kuahirishwa kwa uchaguzi wa ugavana kaunti hiyo na Kakamega baada ya karatasi za kura kupatikana na dosari.

Bila shaka, wagombeaji ugavana Mombasa sasa watalazimika kutia bidii ili kuhakikisha idadi kubwa ya wapigakura watajitokeza katika uchaguzi huo.

Mwanzo kabisa, kinyang’anyiro cha kurithi kiti cha Gavana Hassan Joho, anayekamilisha kipindi chake cha pili uongozini, kilikuwa kimevutia ushindani mkali na kusisimua siasa za jimbo hilo.

Wagombeaji waliokuwa kifua mbele walikuwa mfanyabiashara Suleiman Shahbal, Mbunge wa Kisauni anayeondoka, Bw Ali Mbogo, mwenzake wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir na seneta wa zamani wa Mombasa, Bw Hassan Omar.

Baadaye, aliyekuwa gavana wa Nairobi, Bw Mike Sonko, alijitosa ulingoni muda mfupi kabla mlango wa uteuzi wa wagombeaji kufungwa katika hatua iliyoshangaza wengi.

Bw Shahbal, aliyekuwa akimezea mate tikiti ya ODM, alishawishiwa kumwondokea Bw Nassir, naye Bw Mbogo aliyetaka tikiti ya Wiper, akamwachia nafasi Bw Sonko.

Baada ya vuta nikuvute kati ya Bw Sonko, IEBC na mashirika ya kijamii yaliyopinga ugombeaji wake mahakamani kwa msingi kuwa alitimuliwa Nairobi kwa sababu za kimaadili, mwanasiasa huyo alizimwa.

Pamoja na Bw Mbogo, wakaamua kubadili uaminifu wao wa kisiasa kutoka kwa chama cha muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, wakaelekea kwa Kenya Kwanza na kuunga mkono azma ya Bw Omar.

Kwa baadhi ya wapigakura, matukio haya yote ni ya kukoroga akili mno. Wamerushwa huku na kule kwa muda mrefu hadi dakika ya mwisho.

Minong’ono mitaani ilikuwa tayari inaashiria kuna wale ambao walishakufa moyo kushiriki katika upigaji kura za ugavana kwa vile wale watu waliokuwa wakiwashabikia hawangekuwa tena debeni.

Wengine wao waliweza kushawishiwa kwamba bado kuna nafasi kuchagua viongozi wengine wanaowania ugavana, hasa ikiwa wangeenda katika vituo vya uchaguzi kuchagua wagombeaji wa viti vingine ambavyo ni urais, useneta, ubunge, udiwani na uwakilishi wa kike bungeni.

Wanaohamasisha wakazi kuhusu upigaji kura wasifunge kazi ikiwa walishapanga kufanya hivyo. Bado kazi ipo kuwashawishi wakazi wa Mombasa kuhusu umuhimu wa kujitokeza kwa wingi kujiamulia gavana wa pili wanayemtaka kuwaongoza kwa miaka mitano ijayo.

  • Tags

You can share this post!

Mwanamke anyakwa akiwa na manoti kituoni

Benzema aongoza Real Madrid kukomoa Eintracht Frankfurt na...

T L