VALENTINE OBARA: ODM ijipige msasa ndipo iweze kuendelea kudhibiti Mombasa

VALENTINE OBARA: ODM ijipige msasa ndipo iweze kuendelea kudhibiti Mombasa

NA VALENTINE OBARA

CHAMA cha ODM kina kila sababu ya kujipanga upya ikiwa kitaendelea kudhibiti ufuasi wake katika Kaunti ya Mombasa.

Ingawa viongozi wa chama hicho na baadhi ya wafuasi wanasherehekea jinsi kilivyofanikiwa kushinda viti vyote isipokuwa kimoja cha ubunge pamoja na useneta, kiti cha mbunge mwakilishi wa kike na idadi kubwa ya madiwani, matokeo ya uchaguzi wa urais yanaonyesha hali si shwari kwa chama hicho cha Bw Raila Odinga.

Kwa mujibu wa matokeo ya kura za urais yaliyochapishwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Bw Odinga, aliyewania urais kupitia chama cha Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, alipata kura 161,015 Mombasa, ambazo ni sawa na asilimia 58 ya kura zilizopigwa.

Kwa upande mwingine, mpinzani wake wa karibu, Dkt William Ruto, aliyewania kupitia Chama cha UDA, alipata kura 113,700 ambazo ni sawa na asilimia 41 ya kura zilizopigwa.

Hii inaonyesha kuwa, tofauti na ilivyokuwa katika chaguzi zilizopita ambapo kulikuwa na tofauti kubwa ya kura kati ya Bw Odinga na wapinzani wake, wakati huu pengo lilikuwa dogo mno.

Tofauti ya kura alizopata Bw Odinga katika Kaunti ya Mombasa dhidi ya Dkt Ruto ilikuwa ni 47,315 au asilimia 17 pekee.

Hali hii ni tofauti na kaunti nyingine za Pwani zilizo na idadi kubwa ya wapigakura ambazo ni Kilifi na Kwale ambapo kinara huyo wa ODM alipata kura zaidi ya asilimia 70, huku Dkt Ruto akipata chini ya asilimia 30 ya kura zilizopigwa.

Hii ni licha ya kuwa, katika kaunti hizo mbili, ODM ilipoteza baadhi ya maeneobunge iliyokuwa imeshikilia awali na vilevile, ikapoteza katika uchaguzi wa ugavana Kwale.

Ingawa uchanganuzi wa kina utahitajika kubainisha kiini cha hali hii, kuna uwezekano mipangilio duni ya kampeni za urais Mombasa ilichangia matokeo hayo.

Katika kipindi kizima cha kampeni, kuliibuliwa shaka baina ya wadadisi wa kisiasa kuhusu jinsi hapakuwa na kampeni zozote za kuridhisha za ODM katika Kaunti ya Mombasa.

Baadhi ya wadadisi walitaja kukosekana kwa Gavana Hassan Joho, kama chanzo cha ukosefu wa kampeni zilizokuwa zimezoeleka miaka iliyopita kwa kuwa gavana huyo alitumia muda wake mwingi kumpigia debe Bw Odinga nje ya Mombasa.

Kampeni za ODM zilizofanyika mjini humo ambazo ziliongozwa na Bw Odinga zilikuwa chache ikilinganishwa na zile za Dkt Ruto na wafuasi wake.

Katika ukanda mzima wa Pwani, Kaunti ya Mombasa hutazamwa kama makao makuu kwa vile ni kiingilio kikuu, sio tu kwa kaunti zingine za ukanda huo bali cha kitaifa na hata kimataifa kwa sababu ya uwepo wa bandari na uwanja mkuu wa ndege.

  • Tags

You can share this post!

Serikali kutoa mwelekeo wa kalenda ya masomo

KINYUA BIN KING’ORI: Chebukati ashamaliza kazi yake,...

T L