VALENTINE OBARA: Tujihadhari sana Pwani isigeuke kuwa Sodoma

VALENTINE OBARA: Tujihadhari sana Pwani isigeuke kuwa Sodoma

Na VALENTINE OBARA

WASWAHILI husema, mgeni njoo mwenyeji apone. Kama kauli hii ingekuwa ikitimiwa kikamilifu, hakika maeneo ya Pwani yaliyo na vivutio vikuu vya utalii, yangekuwa yamepata manufaa makubwa kuliko jinsi ilivyo kwa sasa.

Lakini hali sivyo, kwani mbali na manufaa ambayo yameletwa tangu jadi na watalii wanaozuru Pwani, kuna maovu ambayo pia yametokea wakati wafanyabiashara walafi wanapojaribu kila mbinu kuvutia watalii kwa vilabu vyao.

Maovu hayo yanajumuisha visa kama vile dhuluma za kingono dhidi ya watoto, ulanguzi wa dawa za kulevya, ukahaba, ushoga na hata majaribio ya vitendo vya ugaidi.

Hivi majuzi, ilibainika kuwa malefu ya kesi za dhuluma dhidi ya watoto huripotiwa kila mwaka Pwani, kwa mujibu wa tafiti za shirika la Global Fund to End Modern Slavery (GFEM).

Vilevile, kumekuwa na kesi nyingi zinazohusu raia wa kigeni ambao hukamatwa wakiwa na dawa za kulevya, huku wengine wakinaswa na vifaa vya kutengeneza vilipuzi ambavyo huaminika ni kwa mipango ya kutekeleza ugaidi ndani ya nchi.

Jamii za Pwani zinahitaji kujihadhari sana na masuala kuhusu kuhadaa watoto ili waingilie maovu, na lile la ulanguzi na utumizi wa dawa za kulevya miongoni mwa maovu mengine.

Iwapo wadau husika katika sekta ya utalii, usalama na haki za watoto wataendelea kufumbia macho dhuluma dhidi ya watoto, kuna hatari ya kufanya liwe mojawapo ya vivutio vikuu vya utalii Pwani katika miaka ya usoni.

Huu ni mwelekeo ambao umewahi kutokea katika baadhi ya nchi za mabara tofauti kama vile Asia na Ulaya, ambapo watalii huenda tu kutafuta uhuru wa kunyanyasa watoto wa kike na wa kiume.

Baadhi ya watoto hao huwa wametekwa nyara na makundi ya wahalifu ambao hulipwa kupelekea wafanyabiashara kama vile wa vilabu na madanguro, huku wengine wakiwa wamepelekwa na wazazi wao ambao hupokea malipo kwa unyama huo.

Mbali na hili, kuna pia mataifa ambayo utumizi wa dawa za kulevya umebadilishwa kuwa kivutio kikubwa cha utalii.

Katika mataifa aina hiyo, karamu za aina mbalimbali huandaliwa kwa mfano katika vilabu vya kitajiri ambapo mihadarati huuzwa.

Mbali na kuwa aina hii ya utalii husababisha kero la usalama ikizingatiwa mizozo ambayo huibuka baina ya magenge ya walanguzi wa dawa za kulevya, athari nyingine ni kiwango kikubwa cha dawa hizo huingizwa mitaani na kufikia wenyeji hasa vijana.

Kufikia sasa, athari za dawa za kulevya kwa vijana wa Pwani si jambo la siri kwa hivyo hatua yoyote inayoweza kuchangia ongezeko la kusambaza mihadarati ni sharti ikomeshwe mara moja.

Kukomesha mbinu hizi mbovu za kuvutia watalii Pwani kutafanikishwa tu kupitia kwa ushirikiano wa wadau wote., kuanzia kwa jamii, viongozi wa mashinani hadi afisi za serikali ya kitaifa.

Bila hilo, ipo siku ambapo tutaamka na kugutuka kuwa ukanda huu umebadilika kuwa kitovu kikuu cha kila aina ya maovu kuliko jinsi ilivyo sasa.

  • Tags

You can share this post!

Viongozi wa kanisa warudishia mbunge pesa alizochangisha

GWIJI WA WIKI: Ali Salim M’Manga

T L