VALENTINE OBARA: Wanaomezea ugavana wajue kazi yahitaji maono

VALENTINE OBARA: Wanaomezea ugavana wajue kazi yahitaji maono

NA VALENTINE OBARA

MWAKA huu idadi kubwa ya wabunge wanatarajia kujitosa katika shindano la kuwania ugavana katika kaunti mbalimbali nchini.

Orodha ndefu ya wabunge hao inajumuisha baadhi kutoka kaunti za Pwani, kama vile Bi Aisha Jumwa ambaye ni Mbunge wa Malindi, Bw Abdulswamad Nassir (Mvita), Ali Mbogo (Kisauni) miongoni mwa wengine ambao bado hawajajitokeza kwa ukakamavu kueleza maazimio yao.

Kinachojitokeza katika kampeni za wabunge hao ni kuwa, wengi wao wanajipigia debe kwa msingi wa utendakazi wao wa sasa.

Inabainika kuwa mojawapo ya vigezo vikubwa ambavyo wanataka wananchi wazingatie ili kuwaweka mamlakani ni jinsi walivyosimamia matumizi ya hela za Hazina ya Serikali ya Kitaifa ya Kustawisha Maeneobunge (NG-CDF).

Ni bayana kwamba kuna baadhi ya wabunge wanaotaka kuwania ugavana ambao kweli walisimamia vyema pesa za CDF kwa manufaa ya umma na hivyo basi wana haki kutumia suala hilo kujipigia debe kama viongozi waliodhihirisha wanajali maslahi ya wananchi.

Hata hivyo, inafaa ieleweke kuwa usimamizi wa kaunti unahitaji kiongozi ambaye anaweza kutenda mengine mengi zaidi kuliko hilo.

Majukumu ya gavana ni makubwa zaidi kwa hivyo mafanikio ya usimamizi wa hazina ya eneobunge pekee hayatoshi kuwa kishawishi cha uwezo wa mtu kuongoza kaunti ipasavyo.

Tangu uongozi wa mfumo wa ugatuzi ulipoanza kutekelezwa humu nchini mwaka wa 2013, kuna changamoto nyingi ambazo zimeonekana katika karibu kaunti zote.

Ni kaunti chache mno kati ya 47 zilizopo ambazo zimefanikiwa kiasi cha haja kudhibiti mawimbi makali yaliyoshuhudiwa katika kipindi hicho kwa sababu ya uongozi bora.

Changamoto kuu zilizotokea katika kaunti nyingi ni kama vile kutokamilishwa kwa ujenzi wa miundomsingi muhimu, mazingara duni ya utendakazi kwa wafanyakazi wanaotoa huduma muhimu kwa umma kama vile za afya, ufujaji wa pesa za umma, ukosefu wa maono mapya uongozini ambayo yanaweza kufaidi umma kama vile kwa kuongeza nafasi za ajira, miongoni mwa mengine.

Mambo mawili makuu ambayo hujitokeza katika changamoto hizi ni kuhusu fedha na uongozi duni.

Kuhusu fedha, matatizo huwa yanasababishwa na ukosefu wa fedha, usimamizi mbaya wa fedha na ufisadi.

Kwa upande mwingine, uongozi duni ni ule usiokuwa na maono yoyote mapya ambayo yanaweza kusaidia umma kama vile kwa kupanua nafasi za ajira.

Itakuwa vyema kama kila kiongozi anayepanga kuwania ugavana atahakikisha ameeleza wazi jinsi anavyopanga kushika usukani wa safina ya kaunti kuvuka mawimbi haya bila kuzama kwani kuzama kwake kutazamisha matumaini ya wananchi.

Haitoshi kueleza wananchi kwamba kiongozi amebobea katika usimamizi wa eneobunge kwa miaka mingapi, wala kusimamia biashara kubwakubwa kwa miongo mingapi.

Kile ambacho mwananchi anafaa kuthibitishiwa ni jinsi uongozi wa kaunti utakavyoleta mafanikio yaliyonuiwa wakati raia walipoamua kupitisha Katiba ya kuunda mfumo wa utawala wa ugatuzi.

  • Tags

You can share this post!

Waathiriwa wa fujo Lamu kukosa kushiriki uchaguzi

TAHARIRI: Serikali iunde sera wakongwe wafunze vijana...

T L