Dondoo

VALENTINO DEI: Buda atupiwa maji taka asiende kwa kimada

February 13th, 2020 1 min read

Na MWANDISHI WETU

KITENGELA MJINI

K ALAMENI mmoja mjini hapa alijipata taabani baada ya kumwagiwa maji taka na mkewe ili asiende kukutana na kimada wake Valentino Dei.

Mkewe alikuwa amesoma arafa kadhaa kwa simu ya mumewe na akabaini kwamba siku hiyo alikuwa ameagana na mwanadada mmoja wakutane mjini hapa.

Saa ya kuondoka ilipofika, jamaa alijiandaa kwenda kuonana na kimada wake.Alidai kwamba alikuwa na shughuli nyingi na hangerudi nyumbani mapema.

Hapo ndipo mkewe alipoamua kuchukua nguo zake na kuzitupa kwa maji na kumkabili.? “Ninajua uendako, ikiwa wewe ni mwanamume kamili, jaribu kutoka nje ya mlango huo ukione cha mtema kuni,” mama alimuonya jamaa.

Na kama masikio ya kalameni yalikuwa na pamba, alielekea moja kwa moja hadi mlangoni.Inasemekana mkewe alichukua besheni iliyojaa maji taka aliyokuwa ameweka baada ya kuosha vyombo.

“Mara ya mwisho! Jaribu kutoka uone!” mke alifoka.

Kulingana na mdokezi, jamaa hakujali. “Mkewe aliinua besheni na kumrushia maji taka yote akachafua nguo alizokuwa amevaa. Jamaa hakuamini kamwe. Alikimbia chumba cha? kulala kubadilisha mavazi lakini akapata yote yalikuwa kwenye beseni kadhaa yakiwa yamelowa maji,” alieleza mdokezi.

Jombi alisikika akifadhaika baada ya kugundua kwamba alikuwa amebanwa. Kimada wake aliendelea kumpigia simu ili wakaburudike Valentino Dei bila kusita lakini hakumpata.

Mwanadada huyo hakujua kwamba mipango ya jamaa ilikuwa imezimwa. Simu ya jamaa pia ilikuwa imeingia maji na kuzimika.

Jamaa alilazimika kubaki nyumbani akiwa amejifunga taulo kiunoni.? Kulingana na mdokezi, mkewe aliapa kumchukulia hatua kali zaidi akiendelea kuhanya.

Hata hivyo, haikubainika iwapo jamaa aliacha tabia hiyo kufuatia vitisho vya mkewe.