Afya na Jamii

Valentino: Wanaume wenye mabibi wengi wataka hakikisho SHIF itawajali

February 14th, 2024 1 min read

NA MAUREEN ONGALA

WANAUME wenye wake kuanzia wawili kuendelea wameitaka Wizara ya Afya kueleza namna ambavyo familia zao zitafaidika moja kwa moja na mpango mpya wa huduma ya Bima ya Kijamii ya Afya (SHIF) ambayo inajaza nafasi ya Bima ya Kitaifa ya Afya (NHIF).

Kulingana na wanaume hao, familia zao zilipitia changamoto nyingi kwa sababu sheria ya NHIF ilikuwa na kikwazo na pingamizi kubwa kwao kupata matibabu na huduma nyingine za afya.

Akizungumza katika kikao cha kukusanya maoni kuhusu SHIF katika hoteli moja mjini Kilifi, Mzee Juma Mbarak alisema Waislamu wameathirika pakubwa ikizingatiwa dini imewaruhusu kuwa na hata wake wanne.

Bw Mbarak alisema NHIF iliruhusu mke mmoja kupata huduma za afya.

“NHIF ilizuia familia zetu kupata matibabu na kutulazimisha kulipia pesa taslimu kila mara wake zetu walipoenda hospitalini kutibiwa,” akasema Bw Mbarak.

Alitaja hali hiyo kuwa ya ubaguzi na kusema inaleta picha mbaya katika jamii na pia changamoto nyingi wakati wa kutafuta matibabu ikizingatiwa familia myingi hazina fedha za kutosha kugharimia matibabu ambayo wakati mwingi huwa ghali mno.

“Hili si  jambo nzuri. Tunataka serikali itilie maanani kuwa dini ya Kiislamu kuwa inaruhusu mwanamume kuoa mabibi wengi na pendekezo bora ni kuwa wake wote wajumuishwe katika bima ya SHIF,” akasema.

Kiongozi wa wazee wa mtaa katika kata ya Kilifi Township Bi Aisha Said alitaka wizara kuwatuma maafisa nyanjani ili kuelimisha  jamii zaidi kuhusu bima hiyo mpya.

Bi Said alieleza kuwa watu wengi bado wanakumbukumbu mbaya ya NHIF kufuatia changamoto walizopitia na kuna umuhimu wa wao kuwa na ufahamu wa kutosha.

“Mambo ya huko nyuma bado yanatafuna watu na ndio sababu watu wengi waliohudduria kikao hiki cha kutoa maoni wanaelezea kumbukumbu zao kwa sababu wengi walikuwa hawapati matibabu ya sawa,” akasema Bi Said.

[email protected]