Michezo

Valverde asema hawazii kujiuzulu Barca baada ya kuondolewa UEFA

May 13th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

KOCHA wa Barcelona Ernesto Valverde amesema kwamba hajawahi kuwazia kujiuzulu tangu klabu hiyo ibanduliwe kwenye kipute cha Klabu Bingwa Barani Ulaya (Uefa) na Liverpool.

Mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Uhispania (Laliga) walichapwa 4-0 na Liverpool ugani Anfield Mei 7, 2019 na kufurushwa kwenye mashindano hayo kwa jumla ya mabao 4-3.

Ingawa Barcelona imetawala mashindano ya nyumbani baada ya kushinda ligi na Supercopa de Espana mwanzoni mwa msimu, kocha Valverde amekuwa akimulikwa kwa kutowatambisha kwenye mechi za Bara Uropa kama watangulizi wake.

Mabingwa hao walijipata katika hali kama hiyo msimu wa 2017/18 walipoondolewa na As Roma ya Italia kwa kuchapwa 3-0 hata baada ya kushinda mechi ugani Camp Nou. 4-1.

“Sijawazia kuwacha kazi hii,” Valverde akawaeleza wanahabari baada ya kushuhudia Barcelona ikiichapa Getafe 2-0 Jumapili Mei 12.

Wakati wa mechi hiyo mashabiki waliwazomea Philipe Countinho na Sergio Basquets kwa kuchangia kichapo walichopokezwa na Liverpool.

“Nilitarajia watuzomee lakini hayo ni kawaida kwa mashabiki timu inapokosa kufikia malengo yao uwanjani. Hata hivyo tunashukuru kwa uungwaji mkono na sifa wanazotumiminia tukishinda mechi muhimu,” akaongeza Valverde.

Barcelona wanatamatisha msimu wa La Liga kwa mechi ya ugenini dhidi ya Eibar Jumapili Mei 19 kisha wakabiliana na Valencia kwenye fainali ya Kombe la Copa del Rey mnamo Jumamosi Mei 25.