Michezo

Van Dijk ana kila sababu ya kunyakua Ballon d’Or

July 28th, 2019 2 min read

NA CHRIS ADUNGO

BAADA ya kuongoza Liverpool kutawazwa wafalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), beki Virgil van Dijk wa Uholanzi alitawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu jana.

Mholanzi huyu kwa sasa anapigiwa upatu wa kunyanyua taji la Ballon d’Or ambalo Mchezaji Bora zaidi duniani hupokezwa Disemba ya kila mwaka baada ya wawaniaji kuorodheshwa Oktoba.

“Iwapo nitatuzwa kwa sababu ya msimu niliojivunia kambini mwa Liverpool muhula uliopita, basi itakuwa tija na fahari tele,” akasema Van Dijk.

Wanne kati ya masogora sita wanaopigiwa upatu wa kunyakua taji la Ballon d’Or ni wachezaji wa Liverpool. Mbali na Van Dijk anayetarajiwa kuwatoa Lionel Messi na Cristiano Ronaldo kijasho, wengine waliopo mstari wa mbele ni Mohamed Salah, Sadio Mane na kipa Alisson Becker.

Kihistoria, taji la Ballon d’Or lilikuwa likibadilisha mikono kati ya Messi na Ronaldo ambao wanajivunia kutia kapuni ubingwa huo mara tano kila mmoja kati ya 2008 na 2017.

Hata hivyo, ukiritimba huo ulipigwa breki mwaka jana baada ya kiungo Luka Modric kutawazwa kutokana na ushawishi uliowashuhudia waajiri wake Real Madrid wakinyakua taji la UEFA huku timu yake ya taifa ya Croatia ikitinga fainali ya Kombe la Dunia nchini Urusi.

Kati ya washindi wa hivi karibuni wa Ballon d’Or, wengi wamekuwa wavamizi au viungo wapakuaji ambao wamewahi kuongoza vikosi vyao kunyanyua ubingwa wa UEFA.

Beki wa mwisho kunyanyua taji hili ni Fabio Cannavaro aliyeongoza timu yake ya taifa ya Italia kutawazwa mabingwa wa dunia mnamo 2006. Tangu wakati huo, tisa kati ya washindi 12 (Kaka, Ronaldo, Messi na Modric) waliwahi kutawazwa washindi wa Ballon d’Or baada ya vikosi vyao kutwaa ubingwa wa UEFA.

Upekee umewahi kutokea mara mbili tu ambapo Messi aliibuka mshindi baada ya kupachika wavuni jumla ya mabao 60 mnamo 2010 na magoli 91 mnamo 2012 huku Ronaldo akipepea baada ya kutikisa nyavu mara 66 mnamo 2013.

Hapana shaka kwamba Van Dijk atatawazwa bingwa wa mwaka huu iwapo mfumo ambao umekuwa ukitumiwa katika miaka ya hivi karibuni utadumishwa katika mchakato wa kutafuta mshindi kwa mara nyingine.

Ushawishi wa mchezaji katika soka ya UEFA ni kigezo ambacho kimekuwa kikitumiwa sana. Tangu aagane na Southampton mnamo Disemba 2017 na kuingia katika sajili rasmi ya Liverpool kwa kima cha Sh9.7 bilioni, ushawishi wa Van Dijk umekuwa ukihisika sana.Msimu jana, Van Dijk aliwajibishwa katika michuano yote ya Liverpool kwenye kampeni za EPL zilizoshuhudia kikosi hicho cha kocha Jurgen Klopp kikifungwa mabao 22 pekee.

Idadi hii ya magoli ndiyo ndogo zaidi kwa kikosi chochote cha EPL katika orodha ya sita-bora jedwalini kuwahi kufungwa.

Ukubwa na upekee wa Van Dijk kambini mwa Liverpool uliwezesha kikosi hicho kutia kibindoni jumla ya pointi 97, moja pekee nyuma ya Manchester City waliohifadhi ufalme wa taji hilo.

Kikubwa zaidi kinachojivuniwa na Van Dijk ni kutopigwa chenga na mchezaji yeyote wa timu pinzani katika jumla ya mechi 64 zilizopita akivalia jezi za Liverpool. Hii ni rekodi ambayo amekuwa akiishikilia tangu Machi 2018.

Zaidi ya kuwatambisha Liverpool msimu jana, Alisson aliwasaidia Brazil kutia kibindoni ubingwa wa Copa America mwezi huu. Kipa huyu ambaye ndiye ghali zaidi duniani, anajivunia rekodi ya Kupiga jumla ya mechi tisa bila ya kufungwa bao katika ngazi ya klabu na timu ya taifa.

Alisson aliyesajiliwa kutoka Roma kwa Sh8.7 bilioni, alipangua alikosa kufungwa katika jumla ya mechi 21 msimu jana.