Van Dijk athibitisha kwamba hatachezea Uholanzi kwenye fainali za Euro

Van Dijk athibitisha kwamba hatachezea Uholanzi kwenye fainali za Euro

Na MASHIRIKA

BEKI wa Liverpool, Virgil van Dijk amesema kwamba hatakuwa sehemu ya kikosi kitakachotegemewa na timu ya taifa ya Uholanzi kwenye fainali za Euro 2020 zilizoahirishwa.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 29 bado hajapona jeraha la goti baada ya kufanyiwa upasuaji mnamo Oktoba 2020.

“Nahisi kwamba ni maamuzi bora kutocheza Euro na badala yake kushiriki mazoezi mepesi yatakayochangia kupona kwangu kadri ninavyojiandaa kwa kampeni za muhula ujao wa 2021-22,” akasema nahodha huyo wa timu ya taifa ya Uholanzi.

“Japo ni maamuzi magumu, nahisi kwamba yatanifaa,” akaongeza Van Dijk.

Fainali za Euro mwaka huu zimeratibiwa kufanyika kati ya Juni 11 na Julai 11 baada ya kuahirishwa kwa mwaka mmoja kutokana na janga la corona.

“Yasikitisha kwamba nitakosa fainali hizi na sitapata fursa ya kuongoza timu yangu ya taifa kwenye kipute hiki muhimu,” akaongeza.

Kutokuwepo kwa Van Dijk katika kikosi cha Liverpool ni kiini cha miamba hao kushindwa kuhifadhi ufalme wao wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu wa 2020-21. Kikosi hicho cha cha kocha Jurgen Klopp kwa sasa kinashikilia nafasi ya tano kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa alama 63, moja nyuma ya nambari nne Chelsea.

Mbali na Van Dijk, Liverpool wamekosa pia huduma za wanasoka Joe Gomez na Joel Matip kwa kipindi kirefu kutokana na majeraha.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Chipukizi William Saliba kuwa kizibo cha beki David Luiz...

Kocha Roy Hodgson kuagana rasmi na Crystal Palace mwisho wa...