Michezo

Van Persie afurahia kiwango cha kiungo Dani Ceballos

August 21st, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

PARIS, Ufaransa

NYOTA wastaafu wa Arsenal, Robin van Persie na Martin Keown wanaamini kiwango cha juu cha Dani Ceballos kitaisaidia klabu hiyo yao ya zamani.

Hii ni baada ya kiungo huyo kung’ara katika mechi dhidi ya Burnley, mwishoni mwa wiki ambapo Arsenal walishinda mabao 2-1 kutokana na mabao ya Alexandre Lacazette na Pierre Emerick Aubameyanga.

Akizungumza kupitia kituo cha runinga Van Persie alisema Ceballos alikuwa hatari katika mechi hiyo. “Nilimfuatilia kwa makini, ni mchezaji mzuri na hakuwa na presha. Arsenal imekosa mchezaji wa aina hiyo kwa muda mrefu,” alisema Van Persie.

Ceballos ambaye alipiga kona iliyochangia kufungwa kwa bao la kwanza na Lacazette alijiunga na Arsenal majuzi kwa mkopo wa mwaka mmoja akitokea Real Madrid.

“Alisaidia kikosi kwa kukimbia kila kona kutafuta mpira, kitu ambacho timu imekikosa kwa muda mrefu. Kila mtu alikuwa akimuangalia uwanjani . Alijiamini, huku akisambaza mipira kila mahali,” alisema Keown.

Ceballos alikuwa katika kikosi cha kwanza cha Real Madrid mara 17 pekee kwenye mechi za ligi kuu ya La Liga.

Lakini katika mechi yake ya kwanza ugani Emirates, nyota huyo alitajwa kuwa staa wa mchezo wakati kikosi hicho kiliibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Burnley.

Katika mechi hiyo, Arsenal walitangulia kupata bao kupitia kwa Lacazette, dakika ya 43, kabla ya Aubameyang kufunga la pili dakika ya 63.

Mbali na Arsenal, nyota huyu pia alikuwa akiwindwa n a klabu za Tottenham na AC Milan ya Italia.

Kocha Mauricio Pochettinho wa Spurs alimtaka Ceballos, sambamba na Giovani Lo Celso wa Real Betis pamoja na kiungo Tanguy Ndombele wa Lyon.

Kuwa kwenye rada

Nyota hao wote walikuwa kwenye rada ya Spurs kuziba pengo la Mido, Mousa Dembele ambaye amejiunga na Guangzhou R&F.

Ceballos alipoitwa kujiunga na timu ya taifa ya vijana wasiozidi umri wa miaka 21 hakuna aliyemtambua, kwa sababu hakuwa na jina barani Ulaya.

Katika michuano hiyo iliyofanyika nchini Poland, Ceballos alikuwa mchezaji wa akiba, lakini baada ya kupewa nafasi, wakufunzi wa timu hiyo walikuja kumuamini.

Licha ya timu yake kutoibuka mabingwa, ndiye aliyetajwa kuwa mchezaji bora wa mashindano hayo.

Itakumbukwa kwamba wakati wa muhula wa usajili uliopita, Madrid ilijaribu kumnasa katika juhudi za kukijenga kikosi, lakini hawakuelewana na maajenti wake.

Katika hali hiyo, kocha Zinedine Zidane alitakiwa kupunguza baadhi ya nyota wake ambao ni muhimu katika mpango wake wa msimu huu.