Michezo

Van Persie ataka Ole Gunnar apewe muda zaidi

May 22nd, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

MSHAMBULIZI wa zamani wa Manchester United Robin van Persie anaamini kwamba mkufunzi Ole Gunnar Solskjaer atatamba Old Trafford iwapo atapewa muda wa kuifunza timu hiyo badala ya kukemewa kila mara anapopoteza mechi.

Solskjaer alipokezwa kandarasi ya miaka mitatu kama kocha wa Man U ingawa uwezo wake wa kuleta ufanisi ndani ya klabu umeanza kutiliwa shaka baada ya kuchapwa kwenye mechi kadhaa kabla ya kukamilika kwa msimu wa Ligi ya Uingereza(EPL) 2018/19.

Van Persie ambaye alikuwa sehemu ya kikosi cha Man United kilichoshinda EPL mara ya mwisho msimu wa 2012-13, anaamini Solskjaer anafaa kupewa muda na mashabiki ili asajili matokeo yatakayoiwezesha klabu hiyo kushinda taji kwa mara nyingine.

“Nafikiri Solskjaer hana shida ila bahati mbaya. Miaka ya nyuma ilikuwa kawaida kwa mameneja kupewa muda kuleta matokeo mazuri klabuni lakini siku hizi mashabiki wanakata tamaa ukipoteza mechi sita pekee na kukubebea mabango ubanduke

“Ni kinaya kwamba alipoanza kuifundisha Man United kila mtu alikuwa amefurahi. Timu ilikuwa ikishinda na hata kushuhudia miujiza kwa kuibandua PSG kwenye kipute cha Klabu Bingwa Barani Ulaya(Uefa). Kila mtu alitoa wito apokezwe kazi ya kudumu ila wakamgeuka baada ya kusajili matokeo yasiyoridhisha hasa msimu ukikamilika,” akasema Van Persie.

Mshambulizi huyo wa zamani wa Arsenal hata hivyo alisema kwamba Manchester United itaamka msimu ujao wa 2019/20 na itatoa upinzani mkali kwenye mbio za kutwaa ubingwa wa EPL na mashindano mengine.