Michezo

VAR yaongeza ladha ya Afcon

February 8th, 2024 2 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

MASHABIKI wanaofuatilia kwa karibu michuano ya Taifa Bingwa Afrika (Afcon 2023) nchini Cote d’Ivoire wameridhishwa na umuhimu wa mtambo wa Refa Msaidizi wa Video (kwa kifupi VAR) tangu kipute hicho kianze Januari 13, 2024.

Kutokana na usaidizi wa VAR, timu kubwa zenye ushawishi mkubwa ambazo zilitarajiwa zingetwaa ubingwa wa kombe hili ziliondolewa mapema.

Miongoni mwa vigogo waliozimwa mapema ni mabingwa watetezi Senegal, Algeria, Morocco, Ghana, Cameroon, na Mali.

Mtambo huu uliobuniwa mnamo 2018 kuonyesha refa kilichotokea katika tukio la mechi kwa kutumia kumbukumbu ya video ulianza kutumika wakati wa Kombe la Dunia nchini Urusi.

Baadaye katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na sasa unatumika katika ligi nyingine maarufu barani Ulaya za La Liga nchini Uhispania, Bundesliga ya Ujerumani, Serie A ya Italia, na Ligue 1 nchini Ufaransa.

Kwa miaka mingi, timu ziligharimu mabao yasiyo halali, lakini tangu uanze kutumika, mashabiki wameshuhudia mabadiliko makubwa viwanjani kwa usaidizi wa mtambo huu.

Katika mashindano yaliyopita yakiwemo ya Afcon, watu hawangeweza kuona matukio, lakini hakuna siri tena!

Hata katika fainali zinazoendelea nchini Cote d’Ivoire, ni waamuzi wachache sana waliofanya makosa, kutokana na sababu kwamba picha za marudio zinaonyesha wazi ikiwa mtu alifunga bao akiwa ameotea, ama kama bao lilikuwa la halali.

Miaka ya nyuma, waamuzi wengi walikuwa na maamuzi ya kupendelea, huku baadhi yao wakichezesha kwa kiwango cha chini, lakini sasa mtambo huu wa VAR umesaidia pakubwa kuweka mambo wazi, kwani waamuzi wanaojaribu kuonea, ushahidi unaonekana haraka kupitia kwa mtambo huo.

Mtambo huu unaonyesha kila kitu hadharani. Pamoja na mitandao ya kijamii, imesaidia sana kuimarisha viwango vya uamuzi uwanjani, kwani walioonekana wakipendelea tayari wamerudishwa nyumbani.

Tangu mtambo huu uanza kutumika, tumeshuhudia waamuzi wachache walioonekana hawana uwezo wa kumudu mechi kubwa.

Kwa mfano Victor Osimhen aliifungia Nigeria bao la pili dakika ya 85 lakini likakataliwa baada ya mwamuzi kuangalia video za VAR na kugundua Percy Tau alichezewa rafu kabla ya mpira huo kumfikia mfungaji.

Katika mechi nyingine, mashabiki walishuhudia waamuzi wakitoa kadi za njano badala ya nyekundi ambapo baada ya kusaidiwa na mtandao huo, walibadilisha uamuzi wao na kutoa kadi nyekundu.

Hata wale wa umri mdogo kama Mkenya Gilbert Cheruiyot wameonekana kama wenye uzoevu mkubwa baada ya mtandao huo kuanza kutumika rasmi. Marefarii wengine kutoka Kenya walio nchini Cote d’Ivoire ni Peter Waweru Kamaku, na Stephen Yiembe.

VAR imeonyesha vitu sahihi na ambavyo si sahihi kusaidia waamuzi waliotoa kadi ya njano sehemu ilipostahili nyekundu.

Ingawa Cheruiyot, Waweru, na Yiembe wanazidi kupeperusha bendera ya Kenya kimataifa, nchini Kenya safari ni ndefu kwa waamuzi wetu wengi ambao hufanya makossa mara kwa mara, huku wachache wakionyesha umakini watu na kupata fuursa ya kuchezesha mechi kubwa za kimataifa.