Michezo

Vardy afunga penalti mbili na kusaidia Leicester kupepeta West Brom 3-0 ligini

September 13th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

JAMIE Vardy alifunga penalti mbili katika kipindi cha pili na kusaidia waajiri wake Leicester City kuwapepeta West Bromwich Albion 3-0 katika gozi la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Septemba 13, 2020.

Baada ya kipa Sam Johnstone kumnyima Harvey Barnes nafasi tatu za wazi katika kipindi cha kwanza, sajili mpya wa Leicester, Timothy Castagne alifungua ukurasa wa mabao kunako dakika 56 baada ya kushirikiana vilivyo na Mbelgiji mwenzake, Dennis Praet.

Vardy ambaye alitawazwa Mfungaji Bora wa EPL msimu uliopita wa 2019-20, aliongezea Leicester bao la pili kunako dakika ya 74 baada ya kuchezewa visivyo na Kyle Bartley.

Vardy, 33, alipachika wavuni bao la pili na la tatu kwa upande wa Leicester katika dakika ya 84 baada ya Dara O’Shea kumwangusha James Justin.

Kiungo James Maddison alitokea benchi katika kipindi cha pili baada ya kuthibitishwa na kocha Brendan Rodgers kwamba alikuwa amepona jeraha la paja.

Kichapo ambacho West Brom walipokezwa kiliendeleza mwanzo mbaya kwa vikosi vilivyopandishwa ngazi kushiriki EPL mwishoni mwa msimu uliopita.

Fulham walipokezwa kichapo cha 3-0 kutoka kwa Arsenal mnamo Jumamosi ya Septemba 12 ugani Craven Cottage kabla ya Liverpool pia kuwazamisha Leeds United 4-3 uwanjani Anfield.

Ushindi wa Leicester ulikuwa mnono zaidi kwa kikosi hicho kuwahi kusajili tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2020.

Ingawa hivyo, kinachosubiriwa kwa sasa ni iwapo wataendeleza uthabiti wao huo hadi mwishoni mwa msimu hasa ikizingatiwa jinsi walivyosuasua katika miezi michache ya mwisho muhula uliopita.

Baada ya kusajili matokeo bora katika nusu ya kwanza ya msimu na kuonekana kufuzu kwa kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), Leicester walitepetea katika mechi 17 za mwisho zilizowashuhudia wakitia kapuni alama 17 pekee baada ya kuibuka washindi katika michuano minne.

Waliambulia hatimaye nafasi ya tano baada ya kupitwa hatimaye na Manchester United na Chelsea walioridhika na nafasi za tatu nan ne mtawalia nyuma ya Liverpool na Manchester City.

Kati ya mabao 23 ambayo Vardy alipachika wavuni msimu uliopita wa 2019-20, 17 yalipatikana kabla ya Sikukuu ya Krismasi.

Katika mahojiano yake na wanahabari mwishoni mwa mechi dhidi ya West Brom, kocha Rodgers alifichua mipango ya kusajili beki matata zaidi atakayeziba pengo la difenda Ben Chilwell aliyejiunga na Chelsea kwa kima cha Sh6.3 bilioni mnamo Agosti 2020.

West Brom wamerejea katika EPL msimu huu baada ya kuteremshwa ngazi miaka mitatu iliyopita.

Kikosi hicho tayari kimetumia kima cha Sh4 bilioni kujinasia huduma za Matheus Pereira, Grady Diangana na Callum Robinson.