Michezo

Vardy na Maddison wabeba Leicester City hadi tatu-bora EPL

December 14th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

JAMES Maddison, 24, alifunga mabao mawili na kusaidia Leicester City kupepeta Brighton 3-0 katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) uwanjani King Power mnamo Jumapili.

Kiungo huyo raia wa Uingereza alicheka na nyavu za Brighton mara mbili katika kipindi cha kwanza baada ya kushirikiana vilivyo na Jamie Vardy aliyefunga pia sekunde chache kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa kipindi cha kwanza kupulizwa.

Vardy aliyekuwa akicheza mechi yake ya 222 kwenye EPL, alifunga bao lake kwa kukamilisha krosi safi aliyoandaliwa na James Justin.

Makipa wa vikosi vyote viwili walijipata katika ulazima wa kufanya kazi ya ziada huku Mat Ryan akimnyima Marc Albrighton nafasi ya wazi ya kufungia Leicester goli la nne. Kasper Schmeichel alijitahidi vilivyo na kupangua makombora mazito aliyovurumishiwa na Alireza Jahanbakhsh na nyota wa zamani wa Arsenal na Manchester United, Danny Welbeck.

Ushindi kwa Leicester uliwapaisha hadi nafasi ya tatu jedwalini kwa alama 24, moja pekee nyuma ya viongozi Tottenham na mabingwa watetezi Liverpool walioambulia sare katika mechi zao za Disemba 13.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa Maddison kuwahi kufunga mabao mawili katika mechi moja ya EPL huku Vardy sasa akifikisha jumla ya magoli 10 kapuni mwake kufikia sasa msimu huu. Leicester hawajawahi kupoteza mechi yoyote dhidi ya Brighton kati ya saba zilizopita.

Ushindi huo unatarajiwa kuipa Leicester ya kocha Brendan Rodgers motisha zaidi ya kupepetana na Everton katika mchuano mwingine wa EPL mnamo Disemba 16 uwanjani King Power. Brighton kwa upande wao watakuwa wageni wa Fulham ugani Craven Cottage.