Makala

VASCO DA GAMA: Kitega uchumi cha Malindi kilicho hatarini kuangamizwa na wavuvi

October 9th, 2018 2 min read

 NA RICHARD MAOSI

NI adhuhuri na niko hapa mjini Malindi na leo nimeamua kuzuru maeneo ya ufuo wa Bahari Hindi. Natembea kwa mguu katika barabara ya Vasco Da Gama iliyojaa vumbi ya changarawe huku jua utosini likinitoa kijasho.

Wakazi hapa wako katika shughuli zao za biashara, hasa nguo na mapambo ya Uswahilini. Kushoto na kulia kuna mikahawa ya kifahari ambako watalii wanaonekana wakijiburudisha kwa vinywaji huku wakifurahia kuchomwa na jua.

Upepo mwanana unanikaribisha kwenye bahari lenyewe na ninapoupunga najutia kuishi maisha yangu yote kwenye maeneo ya bara.

Mnara wa Vasco Da Gama nauona upande wa kushoto. Wavuvi wametapakaa baharini hapa huku kila mmoja akiwa na jahazi na wavu tayari kuvua samaki.

Kwa umbali, taswira ya kupendeza inawakaribisha watalii na wageni wanaofika kuvinjari, bila kujua hali halisi ya makavazi ya mnara huu.

Hapa, utapokelewa na hali ya upweke, kimya, upepo mwanana pamoja na wafanyikazi wanaoshinda kwenye lango kuu kutwa nzima wakitarajia wageni.

Eneo ambako wavuvi wanachimba mawe ya ujenzi karibu na Mnara wa Vasco Da Gama katika ufuo wa Bahari Hindi, Kaunti ya Kilifi. Picha/ Richard Maosi

Ulinzi umeimarishwa katika eneo la bahari linalozingira mnara, isipokuwa baadhi ya watalii wamekuwa wakitumia sehemu hiyo kufika Vasco Da Gama bila kupitia lango kuu wakiepuka ada ya kiingilio.

Wavuvi wanaonekana kucheza mchezo wa paka na panya na maafisa wa baharini.  Lakini Mnara wa Vasco Da Gama sasa uko hatarini kuangamia kutokana na shughuli za wavuvi katika ufuo wa Bahari Hindi hali mbayo hatimaye italemaza shughuli za utalii.

Baadhi ya wavuvi wanakiri kwa Taifa Leo Dijitali kuwa wamekuwa wakichimba mawe ya ujenzi kutoka mnarani.

Japo mnara wenyewe unapatikana mbali na jiji la Mombasa, kilomita 120 kutoka hapa, wakazi wengi wa Malindi hawajui ni turathi ya kitaifa na ndio maana wanauona kama timbo la mawe na kuyachimba ili kujipunguzia gharama za ujenzi wa nyumba.

Wengi niliozungumza nao wanasema kuwa mnara huu haujawafaidi kwa lolote isipokuwa kuwaletea jina kubwa tu. Maendeleo hayaonekani kabisa maana ukumbi wenyewe ni kama umesahaulika.

Wengine hawaoni sababu za kulipia ada ya kiingilio, kutokana na bei nafuu wanayolipishwa na wavuvi kufika mnarani kupitia njia ya mkato ya baharini.

Mawimbi makali yamekuwa yakisomba mchanga, uchafu na vifushi vya mawe yaliyosimama imara tangu karne ya 13 na kuzidi kuumumunya mnara huu.

Wavuvi katika shughuli zao za baharini. Wamekuwa wakisafirisha wakazi na watalii kwa njia ya mkato kufika kwa mnara wa Vasco Da Gama ili kukwepa ada ya kiingilio ya Sh200. Picha/ Richard Maosi

Mmomonyoko wa udongo unaobeba mawe na mchanga mbali na mnara huacha sehemu nyembamba ya kupitia na kulazimu maafisa kuweka mihimili pembeni ili mnara usizame.

“Kisayansi inaaminika ardhi hapa huachana kwa sentimita moja kila mwaka na ndio hatari inayoweka mnara huu pabaya. Pana uwezekano wa kuangamia siku za usoni iwapo serikali haitachukua hatua,” meneja wa operesheni katika makavazi hayo ambaye alidinda kutaja jina lake alisema.

Kulingana na Bi Loyce Kache, mkazi wa Malindi, mnara wa Vasco da Gama kidesturi ulikuwa sehemu ya mwisho ya kusimama kwa mabaharia wakielekea India.

“Ilikuwa ni vigumu kujenga mnara huu Mombasa kutokana na ugomvi kati ya Waislamu na Wakristo wakizozania ishara ya msalaba iliyotiwa juu yake,” Bi Kache alisema.

Hadi walipoafikiana na wakazi wa Malindi isimame katika milki yao ndipo walipotambua ufaafu wake na kuwaelekeza mabaharia katika safari zao.

Vasco da Gama iko chini ya Makavazi ya Kitaifa ya Kenya, baada ya kutengenezwa na Wareno.

“Licha ya kuwa kitega uchumi kwa wavuvi na wapiga picha kama mimi, wengi wetu hufanya kazi hapa kila siku za wiki kujipatia riziki,” alisema Brian Omondi, mpiga picha kutoka kaunti ya Kisumu anayeishi Malindi.

Iwapo serikali ya Kaunti ya Kilifi na ile ya kitaifa zitazidi kuzembea katika kuhifadhi na kuulinda mnara huu dhidi ya hatari hizi, huenda Vasco Da Gama ikasalia kwenye vitabu vya historia tu.