Veemisc ni mwanamuziki anayefanya vizuri pia katika uigizaji na biashara

Veemisc ni mwanamuziki anayefanya vizuri pia katika uigizaji na biashara

NA JOHN KIMWERE

AMEPITIA changamoto nyingi baada ya kuwa yatima akiwa na umri mdogo.

Hata hivyo ni kati ya wasanii wanaokuja wanaolenga makubwa siku zijazo.

Veronicah Muthoni ama ukipenda Veemisc ni mwanamuziki, mwigizaji chipukizi na mfanyibiashara.

”Ingawa nilivutiwa na muziki tangu utotoni mwangu na nilianza utunzi wangu mwaka 2018 sijapiga hatua kubwa,” anasema na kuongeza kuwa amepania kufikia upeo wa mwanamuziki anayetamba kwa kasi nchini Nadia Mukami anayejivunia vibao kama ‘Maombi’ na ‘Si Rahisi.’

Anadokeza anafanya muziki kwa sababu ya mapenzi yake kwa kuzingatia hajafaidi kwa vyovyote.

Binti huyu ambaye hutunga nyimbo za mapenzi anakaribia kutinga umri wa miaka 24. Tayari ametunga nyimbo kumi na kufanikiwa kurekodi tano.

Vibao hivyo vikiwa ‘Nogewa’ na ‘Baki Nawe’ (Alka Production), ‘Umeniweza’ (Meloe Mpire Records), ‘Mapenzi Hisia’ na ‘Ni wewe tu’ (Ddammy Serious Records).

Kwa sasa anafanya kazi na studio ya Meloe Mpire Records inayopatikana eneo la Kasarani, Kaunti ya Nairobi. Anajivunia kuwa fataki ya ‘Nogewa,’ na ‘Baki nawe,’ zimepata mpenyo na kuchezwa kwenye runinga tofauti. Nyimbo hizo zimechezwa KTN kipindi cha Bambika, KBC (Club 1 Extra), Maishamagic East (Gani kali), Y254 (Bounce Nation) na KUTV (Top in Africa live).

Kwenye masuala ya uigizaji anajivunia kushiriki filamu kama: Hello mr Right (Rembo Tv), Njoro wa uber, Selina na Kina zote (Maishamagic East).

Anasema ana kipaji cha muziki anakolenga kujituma kadiri ya uwezo kuhakikisha ndani ya miaka mitano ijayo muziki wake utakuwa umepiga hatua kubwa nchini.

Anashikilia kuwa muziki wa Kenya unaweza kufanya vizuri lakini ni sharti wanamuziki wajitume kiume pia serikali iwape sapoti vizuri.

”Katika mpango mzima nitakuwa mwenye furaha wakati kazi yangu itakapokubali na nianze kuona faida yake,” anasema.

Nchini Kenya anavutiwa na wasanii kama Juliet Miriam Ayub maarufu Jovial aliyetunga fataki kama ‘Jeraha’ na ‘Unanikosha’.

Pia Nadia Mukami kati ya waimbaji wanaofanya vizuri aliyeghani vibao kama ‘Maombi,’ na ‘Si Rahisi’.

Kwa wasanii wa Bongo anavutiwa nao Nandy na Zuchu watunzi wa vibao kama ‘Siwezi,’ ‘Nimekuzoea,’ na ‘Sukari,’ ‘Wana’ mtawalia.

”Ningependa sana kufanya kulabo na wasanii waliopiga hatua Afrika Mashariki kama Zuchu kati ya waigizaji waofanya vizuri nchini Tanzania,” anasema.

Veronicah Muthoni ama ukipenda Veemisc ni mwanamuziki na mwigizaji. PICHA | JOHN KIMWERE

Kama ilivyo kawaida kwa wasanii wengine wanaoibukia dada huyu anasema kuwa ukosefu wa dedha kugharamia shughuli za muziki wake ni donda sugu.

”Muziki una shughuli nyingi hauwezi kufanya kila kitu maana kando na kurekodi unahitaji kundi la kufanya kazi nalo ambapo bila hela hauwezi kuwa nalo,” anasema na kuongeza sio mteremko kwa msanii kufanya vizuri.

Anahimiza chipukizi wenzake bila kuweka katika kaburi la sahau wasanii waliowatangulia kuwa bni vyema kushirikiana kufanya kazi ya muziki.

”Ni vyema tukome kuwa na wivu wakati wenzetu wanapofanya vizuri bali kila mmoja anapaswa kuunga mkono mwenzake,” akasema.

Mrembo huyu alizaliwa eneo la Nyahururu Kaunti ya Laikipia. Shule ya Msingi alisomea Karungubii Academy kisha kujiunga na Shule ya Upili ya Mwenje.

  • Tags

You can share this post!

Mkataba sasa waanika unafiki wa Naibu Rais

TUSIJE TUKASAHAU: Dkt Ruto atuambie mradi wa kiwanda cha...

T L