Habari

Viagra huangamiza Saratani – Utafiti

April 19th, 2018 1 min read

Na AGEWA MAGUT

KANDO na kupandisha ashiki za kimapenzi, imebainika kuwa dawa za viagra zina uwezo wa kupunguza makali ya maradhi ya saratani.

Utafiti wa hivi punde unaonyesha uwezekano wa viagra kutibu kansa ya ngozi, matiti na ubongo.

Utafiti huo ulichapishwa katika mradi wa Repurposing Drugs in Oncology (ReDO) ambao ni ushirikiano kati ya Hazina ya Kupambana na Kansa kutoka nchi ya Ubelgiji na GlobalCures kutoka Marekani.

Kulingana na utafiti huo uliochapishwa Aprili 11, tiba hiyo iligunduliwa wakati mzee wa miaka 80 aliyekuwa akiugua kansa alipoonyesha dalili ya kupona ugonjwa huo baada ya kuanza kutumia viagra ili kupata ashiki ya kufanya mapenzi.

Pia utafiti huo unasema wanaume wanne katika kliniki moja walionyesha dalili za kupona kansa baada ya kuanza kutumia viagra. Kemikali inayotibu kansa ambayo inapatikana ndani ya viagra huitwa PDE5 inhibitors.

Haitakuwa mara ya kwanza kwa dawa kama viagra kutumiwa kwa lengo ambalo halikusudiwa ilipotengenezwa. Viagra hiyo hiyo imewahi kutumiwa kutibu aina ya ugonjwa wa moyo uitwao Angina. Lakini hiyo ilisahaulika na ikawa maarufu kwa kutumiwa na wanaume kuamsha hamu ya kushiriki ngono.

“Hatua zilizopigwa katika matumizi ya Sildenafil maarufu kama viagra ni ya kuvutia mno. Mwanzo ilikuwa tiba ya ugonjwa wa moyo kisha ikawa ya kuamsha hamu ya kushiriki ngono na sasa ni tiba ya kansa,” alieleza Dkt Pan Pantziarka kutoka Hazina ya kupambana na Kansa.

Kwenye chapisho la Utafiti huo imenakiliwa kwamba kemikali ya PDE5 inhibitors inaweza kupenya katika damu iliyoganda kwenye ubongo na kutibu ugonjwa wa kiakili. Hii inawezekana hata katika tiba ya sehemu nyingine za mwili kama Mapafu, Matiti na kwenye Koo.

“Bei ya chini na kutokuwa na sumu nyingi ndizo huchangia dawa hizi kutumiwa na wengi” alinukuliwa moja wa waandishi wa chapisho hilo.