Makala

Viazi vitamu: Vina faida kiafya na huu hapa utaratibu wa kuvipanda

May 28th, 2019 3 min read

Na SAMMY WAWERU

VIAZI vitamu ni miongoni mwa viazi asili vinavyopendwa na wengi nchini na Afrika Mashariki.

Ni vitamu kutokana sukari yake, ya ndani kwa ndani. Aghalabu, huliwa kama staftahi, yaani chakula cha asubuhi.

Aidha, hupikwa kwa njia ya kuchemsha, kuchoma na wengine huvikaanga kwa kuchanganya na viazi mbatata, viazi vikuu (nduma) au ndizi.

Faida kiafya

Ni muhimu kutaja kwamba viazi vitamu ni miongoni mwa vyakula vyenye wanga. Vimesheheni Vitamin A, C, B5, B6, C, na E. Pia, viazi hivi vina madini kama vile; Potassium, Magnesium, Manganese, Iron, Calcium na Zinc.

Ni kiini kizuri cha Beta-Carotene na Choline, viini lishe vinavyosaidia kustawisha ngozi.

Kwa mujibu wa makala ya gazeti la Mwananchi, lililoko nchini Tanzania, na linalomilikiwa na shirika la Nation Media Group, iliyochapishwa mnamo Januari 1, 2018, Beta-Carotene kwenye viazi hivi husaidia kudhibiti maradhi ya moyo, pumu na kupunguza kasi ya mwili kuchakaa.

Gazeti hilo pia limeangazia utafiti uliofanywa na Taasisi ya Chakula na Dawa, Marekani (U.S. FDA), ambao unabainisha kwamba kiazi kimoja kikubwa kinaweza kumpa mtu asilimia 100 ya Vitamini A inayohitajika mwilini kila siku.

Utafiti wa US. FDA pia ulibainisha viazi vitamu vina manufaa sana kwa wanawake wajawazito, na wanaonyonyesha, hasa kutokana na ukwasi wa madini yake.

Ukuzaji

Kuna aina tofauti ya viazi vitamu. Vyekundu juu ndani vyeupe, vyekundu juu ndani manjano, vyeupe juu ndani vyeupe na vyeupe juu ndani manjano.

Kulingana na Bw James Kimemia, mtaalamu na afisa wa kilimo kaunti ya Murang’a ni kwamba viazi vitamu ni rahisi mno kupanda. “Vinastahimili maeneo kame, ndio maana husemekana kuwa mazao bora kuzalishwa sehemu zisizopokea mvua ya kutosha,” aeleza Bw Kimemia.

Havina kikwazo cha udongo vile, kwani vinakua katika udongo wa kichanga (sand) na tifutifu (loam). Hata hivyo, kulingana na mtaalamu huyu wa kilimo, vinastawi vyema katika udongo tifutifu, na kichanga kilichochanganyika na tifutifu.

Njia inayofahamika na kutumiwa na wengi katika upanzi wa viazi hivi ni kwa kuandaa mashimo au mitaro.

Hata hivyo, Bw Kimemia anasema upandaji kwa namna ya kuinua udongo ili kuunda muinuko (ridges), ni rahisi na huongeza kiwango cha mazao.

“Udongo uliochanganywa na mbolea vizuri, uinuliwe kuunda mfano wa mlima hadi karibu futi mbili,” asema mdau huyu, ambaye pia ni mkulima Murang’a.

Mbolea asilia, yaani ya mifugo au ndege kama vile kuku ndiyo bora katika kilimo cha viazi hivi.

Anaendelea kueleza kwamba kutoka mstari mmoja wa mlima hadi mwingine, nafasi inayopaswa kuachwa ni futi nne.

Mbegu ya viazi vitamu ni matawi yake (cuttings) au viazi vyenyewe. Kimemia anapendekeza utumiaji wa matawi, yenye urefu wa karibu futi moja.

Kwenye laini ya muinuko wa udongo, tawi lipandwe kwa kulalishwa (slanting) nusu futi kuenda chini. “Umbali wa tawi hadi lingine uwe futi moja,” ashauri afisa huyu wa kilimo Murang’a.

Wakati wa mahojiano na Taifa Leo katika kijishamba chake wakati wa maonyesho ya kilimo, Mariira Farm, Murang’a, Bw Kimemia alisema viazi vitamu huwa tayari kwa mavuno miezi mitano baada ya upanzi.

Mtaalamu na afisa wa kilimo Murang’a, Bw James Kimemia, wakati wa mahojiano kuhusu kilimo cha viazi vitamu, katika shamba la Mariira. Picha/ Sammy Waweru

Hitaji lake ni maji kwa kipimo, japo ikumbukwa kuwa vinastahimili maeneo kame, ndio maana wakulima huhimizwa kuvipanda kwa wingi ili kuangazia uhaba wa chakula nchini.

Kati ya laini za muinuko wa mchanga, mkulima anapaswa kudhibiti ukuaji wa makwekwe kupitia palizi. Changamoto kuu katika kilimo cha viazi vitamu ni kushambuliwa na fuko.

“Fuko wamenihangaisha, kila viazi vinapoanza kuzaa wanyama hawa huvila na kunisababishia hasara,” analalamika Bi Mary Wairimu, mkulima wa viazi hivi Kirinyaga.

Mapato

Mbali na kutumia dawa ya kuua panya, fuko wanaweza kudhibitiwa kupitia mtego maalum wa kuundwa. Ingawa itagharimu mkulima, kwani kutambua laini wanayoingilia fuko si rahisi.

Viezi vyekundu juu na ndani manjano, kuna aina ya KeMbu 10, KeMbu 20, na Kenspot 4 na Kenspot 2, kwa mujibu wa maelezo ya Bw James Kimemia.

Kulingana naye ekari moja inahitaji matawi 10, 000 kupanda kama mbegu. Ekari moja ina uwezo wa kuzalisha kati ya tani 7 hadi 10 sawa na kilo 7, 000-10, 000. Kilo moja huuzwa kati ya Sh50 hadi Sh100.

Viazi vitamu huwa vimeadimika maeneo ya mjini, hivyo basi mkulima anashauriwa kutafuta namna ya kuimarisha soko lake humo.

“Tunavyopata vinagharimu bei ghali kwa sababu zao hili ni adimu mijini. Wakulima wangeweza kuvikuza kwa wingi na kutuletea, biashara pia yake ingeimarika,” anasema Bw Edwin Kaheti, mkazi wa jiji la Nairobi, na ambaye ni raibu wa viazi hivi.

Kabla ya kuvalia njuga suala la kilimo, mkulima anshauriwa kufanya utafiti wa soko la mazao anayopania kukuza.

Utumizi wa majukwaa ya  mitandao kama vile Facebook na Whats App, pia ni njia mojawapo kufanya matangazo ya mazao.