Habari Mseto

Vibarua wakana kuiba kalamu na karatasi KICC

November 11th, 2020 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

VIBARUA watatu Jumanne walishtakiwa kwa kuvunja na kuiba kutoka afisi ya idara ya huduma za jiji la Nairobi (NMS) kalamu na karatasi zenye thamani ya Sh342,000.

Mabw Benson Musyoka Ikii, Cyrus Elijah Mwanzia na Benjamin Roy Munywoki walikana mashtaka matatu ya kuvunja , kuiba na kupatikana na mali ya wizi mbele ya hakimu mkazi Bi Jane Kamau.

Watatu hao ambao hawakuwakilishwa na wakili walikabiliwa na shtaka kuwa kati ya Novemba 6 na 9 walivunja na kuingia katika afisi za NMS zilizoko katika jumba la mikutano la Kenyatta International Conference Centra (KICC) na kuiba katoni 400 za kalamu za Bic zenye chapa cha NMS na mabunda manne ya makaratasi ya yaliyo na chapa cha idara hiyo inayoongozwa na Meja Jenerali Mohamed Badi . Kalamu zilikuwa 1,600.

Mbali na shtaka hilo la jumla kila mmoja alishtakiwa kivyake kwa kupatikana na baadhi ya bidhaa hizo zilizoibwa kutoka afisi za NMS zilizoko KICC.

Munywoki alikutwa na bunda la makaratasi nao Mwanzia na Ikii wakapatikana na kalamu 400 zenye chapa cha NMS. Waliachiliwa kwa dhamana ya Sh20,000. Kesi itasikizwa Novemba 17.