Habari Mseto

Video ya mtoto mwenye kebehi na matusi yaushtua ulimwengu

September 19th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

HISIA mseto zinaendelea kutolewa na wananchi na viongozi kufuatia video iliyochapishwa mitandaoni mnamo wikendi na mwanafunzi akionekana kutishia mwenzake.

Kwenye video hiyo iliyopakiwa na mwanafunzi wa kiume anayedaiwa kusomea katika shule moja ya msingi eneo la Westlands jijini Nairobi, anasikika akirushia mwenzake wa kike maneno mazito na kumtishia kumpiga risasi.

“Nitachoma dawati na vitabu vyako vyote. Uniepuke kabisa kwa sababu mimi ni hatari, nitakupiga risasi kichwani. Unaniskia; nitakukujia kesho,” inasema video ya kwanza.

Kwenye video ya pili, mtoto huyo anarushia mwenzake cheche za maneno kebehi na dharau na kugusia masuala ya ngono.

Mapema wiki hii, inasemekana makachero kutoka idara ya Uchunguzi wa Jinai (DCI) walifanya mkutano wa faragha na kamati ya shule hiyo.

Licha ya mwanafunzi huyo kwenye video nyingine kuonekana akiomba msamaha na kuililia shule anayosomea isimpige marufuku, baadhi ya wachangiaji katika mitandao wanaendelea kukashifu tabia zake. Pia, wanakosoa wazazi wakidai wameshindwa kuimarisha tabia na maadili hususan kizazi cha kisasa.

“Watoto waliodekezwa, lazima wawe hivyo iwapo wazazi wao si kielelezo chema. Uzazi umeachiwa yaya ambao hawaruhusiwi kukaripia watoto. Na bado,” akasema Josphat Muciocqer.

Esther Maivein anachangia akisema, “Tusilaumu watoto ila wazazi wao. Watoto wanaiga wanayosema wazazi. Wanalaumiwa kwa sababu wanachosema watakiiga siku za usoni.”

Hata hivyo, kuna baadhi ya wachangiaji wanaomsifu wakimtaja kama shujaa. Kimani Ray-e anasema hili si suala linalopaswa kusifiwa, akieleza kwamba “maadili yamemomonyoka kwa watoto wa kileo na tabia za aina hiyo zisisifiwe”.

Mnamo Jumatatu gavana wa Nairobi Mike Sonko alijitokeza na kueleza kwamba mwanafunzi huyo anahitaji msaada. Kwenye ukurasa wake wa Facebook Bw Sonko alichapisha kuwa mvulana huyo anahitaji msaada kwa sababu anang’ang’ana na huenda kuna changamoto fiche anazopitia.

Gavana huyo pia alihimiza Wakenya waitikie msamaha wake akipendekeza aoneshwe mapenzi, kuelekezwa na kupata mashauri nasaha.

Ni kauli ambayo jana iliradidiwa na mbunge wa Suba Kaskazini Millie Odhiambo, akihimiza Wakenya kukoma kusambaza video hiyo.

“Unapoisambaza humfanyi kuwa shujaa. Miaka 20 ijayo mvulana huyo atajutia matamshi yake,” alisema mbunge huyo.

Alisema haja ipo watoto wafahamishwe kuwa vitisho ni hatia kubwa na kwamba wanaweza kushtakiwa katika korti za watoto na kuhukumiwa kifungo.

Bi Odhiambo anapendekeza wazazi na wanafamilia wamtoe mtoto huyo katika mazingira anayokulia, akifafanua kuwa huenda ndiyo yamechangia kumomonyoka kwa tabia na maadili yake. “Wakishindwa, idara ya watoto iingilie kati. Ni wazi kuwa baadhi ya wazazi wamefeli katika majukumu yao ya malezi,” akasema.

Pengo kubwa

Kasisi Charles Kinyua wa kanisa la Katoliki, anasema kudorora kwa maadili ni ishara kuwa kuna pengo kubwa kati ya mzazi na mwanawe.

“Mzazi anapaswa kuwa rafiki wa kwanza na wa karibu kwa mtoto wake. Malezi si kumvisha mavazi, chakula au kumuelimisha pekee. Atengee mwanawe wakati kumshauri maadili mema na namna ya kuishi na jamii,” afafanua Bw Kinyua.

Mitandao ya kijamii kwa upande mwingine inalaumiwa kuchangia kudidimia kwa maadili miongoni mwa watoto, wazazi wakihimizwa kudhibiti wanao katika matumizi yake.

Inashangaza kuona watoto walio chini ya umri wa miaka 18 wakimiliki simutamba na kufungua akaunti za mitandao mbalimbali.

Ni kwenye mitandao hiyohiyo watoto wanatangamana na watu wazima na hata kufuatilia machapisho na video zinazopotosha, na ambazo kilele chake kinakuwa kuchafua maadili yao.