Habari

Video yatarajiwa mahakamani kama sehemu ya ushahidi wa mauaji ya Willie Kimani

October 8th, 2019 1 min read

Na SAM KIPLAGAT

KESI ya maafisa wanne wa polisi na mtu mwingine wanaokabiliwa na mashtaka ya kuwaua kinyama wakili Willie Kimani, mteja wake na dereva wa teksi inaendelea ambapo leo Jumanne video – kuonyesha mahali walipouliwa – ikitarajiwa kuonyeshwa mahakamani.

Video hiyo ya muda wa takribani dakika 41 pia itaonyesha pahala miili ya wahanga wa uhalifu huo ilipatikana; katika Mto Athi River eneo la Donyo Sabuk, Kaunti ya Machakos.

Video hiyo ilinaswa wakati Peter Ngugi, aliyekiri kuhusu jinsi ambavyo mauaji hayo yalitekelezwa, aliwapeleleka maafisa waliokuwa wakichunguza mauaji hayo katika eneo la mauaji katika Mombasa Road karibu na Mlolongo na mto.

Video pia itabainisha jinsi unyama huo ulitekelezwa kwa muda wa takribani saa tatu ambapo Kimani, mteja wake Josephat Mwenda na dereva wa teksi Joseph Muiruri walipoteza uhai mwaka 2016.

Jana Jumatatu, Mkuu wa Kitengo cha Uchunguzi wa Makosa yanayohudu Ardhi, Inspekta Mkuu Geoffrey Kinyua alikuwa katika kizimba cha mashahidi ambapo alitoa ushahidi uliopatikana kwa kumrekodi Ngugi, ambaye ni mmoja wa washtakiwa katika mauaji ya watu watatu hao.

Washukiwa wengine ni Leonard Maina, Sylvia Wanjohi, Stephen Morogo na Fredrick Leliman.