• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 1:51 PM
Mong’are atolewa jasho na digrii yake

Mong’are atolewa jasho na digrii yake

NA RICHARD MUNGUTI

MWANIAJI kiti cha urais aliyetemwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Walter Mong’are alihudhuria masomo ya chuo kikuu kwa miezi saba tu, ilifichuliwa Ijumaa.

Huku Mong’are akidondokwa na jasho jembamba aliposhindwa kueleza jinsi mmoja anavyoweza kufaulu kwa digrii katika muda wa miezi saba.

Wakili wake Dkt Alutalala Mukhwana alishindwa kutetea ushahidi aliowasilisha kuhusu digrii ya Mong’are.

“Mimi siwezi nikajibu maswali kuhusu masomo ya Mong’are katika Chuo Kikuu cha Daystar. Ni msajili tu ama mkufunzi kutoka Daystar anayeweza kufafanua zaidi kuhusu masomo na alama alizopata Mong’are,” alisema Dkt Mukhwana.

Prof Abdi Guliye alimhoji kwa undani jinsi Mong’are alivyohamisha kozi na alama alizopata akiwa Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU) hadi Daystar.

Dkt Mukhwana na Mong’are walisumbuka kueleza kuhusu kizungumkuti cha digrii hiyo ya mwaniaji huyo wa urais aliyetemwa.

Mwaniaji mwingine wa urais Dkt Ekuru Aukot alikaidi sheria za uidhinishwaji akisema “zinakinzana na katiba.”

Wote wawili Dkt Aukot na Mong’are walifukuzwa katika kinyang’anyiro cha urais kwa vile hawakutimiza masharti yaliyowekwa na IEBC.

“Dkt Aukot alikiri hakupata sahihi za wapigakura 48,000 kutoka kwa kaunti 24 zilizomuunga mkono katika azma yake ya kuwania urais,” alisema wakili Moses Kipkogei anayewakilisha IEBC.

Bw Kipkogei alieleza jopo la IEBC linaloongozwa na Mabw Titus Tiego, Profesa Abdi Guliye na Francis Wanderi kwamba Dkt Aukot alisema sheria za IEBC kuhusu uteuzi wa wawaniaji viti zinakinzana na Katiba.

“Dkt Aukot alieleza IEBC kwamba hakutimiza sheria za uteuzi kwa vile zinakinzana na Katiba ambayo ndiyo sheria kuu,” alisema Kipkogei.

Jopo hilo liliombwa litupilie mbali kesi aliyoshtaki Dkt Aukot anayeomba kinara wa muungano wa Azimio Raila Odinga azimwe kuwania Urais Agosti 9, 2022.

Dkt Aukot anadai Azimio si chama cha kisiasa na hivyo hakiwezi kumteua mwaniaji wa urais.

Katika kesi ya Mong’are, Chuo Kikuu cha Daystar kilisema katika ushahidi uliowasilishwa katika jopo la IEBC kwamba mwaniaji huyo alihudhuria masomo kwa muda wa miezi saba tu.

Bw Tiego na wenzake walifahamishwa Mong’are hajahitimu kwa cheti cha digrii.

Bw Mong’are na wakili wake Dkt Alutalala Mukhwana walishindwa kung’amua kinaya jinsi mmoja anavyoweza kuhitimu kwa digrii katika muda wa miezi saba.

IEBC iliomba jopo hilo lihalalishe uamuzi wa IEBC wawili hao hawajahitimu kuwania urais.

  • Tags

You can share this post!

Watu 12,000 wakwama penye vita Ukraine – UN

DOUGLAS MUTUA: Kenya itumie ushawishi wake ipasavyo Afrika...

T L