Kimataifa

Vidosho 30,000 watuma maombi waende ziara mwezini na bwanyenye

January 30th, 2020 1 min read

Na AFP

VIDOSHO 30,000 walituma maombi ya kutaka kuzunguka mwezi na bilionea wa nchini Japan.

Bilionea huyo, Yusaku Maezawa, mnamo Desemba 2019 alitangaza kuwa anatafuta mpenzi atakayeandamana naye katika safari ya kuzunguka mwezi kwa roketi ya SpaceX.

Hata hivyo, bilionea huyo alisitisha shughuli ya kusaka mpenzi huku akisema kuwa amesitisha mpango wa kutaka kuzuru mwezi kutokana na sababu za kibinafsi.

“Nilitamani kwenda kuzuru mwezini lakini nimesitisha ziara hiyo,” akasema bilionea huyo kupitia mtandao wa Twitter.

Akaongezea: “Nasikitika kwamba nimewakwaza wanawake 30,000 waliotuma maombi ya kutaka kuandamana nami mwezini.”

Maezawa, ambaye ni mkurugenzi mkuu wa zamani wa kampuni ya mtandaoni ya mitindo, Zozo, amejizolea umaarufu kutokana na majivuno yake.