Makala

VIDUBWASHA: King’ora cha watoto (Smart Body Temperature Monitor with Wireless Sensor)

September 10th, 2019 1 min read

Na LEONARD ONYANGO

MTOTO anapoangua kilio usiku mambo mawili humjia mzazi akilini: anaweza kuwa mgonjwa au anahisi njaa.

Ni jambo la kawaida kwa wazazi kujihami na dawa ya kupunguza joto kwa watoto wachanga.

Wataalamu wa afya wanasema kwamba mtoto anapopatwa na joto ni ishara kwamba mwili ‘unapigana’ na maambukizi au viini fulani mwilini.

Mtoto anapopatwa na joto usiku na asilie, huenda ikawa vigumu kwa mzazi kujua.

Lakini wataalamu wametengeneza kifaa kinachoweza kukufahamisha mtoto anapopatwa na joto usiku hata ukiwa mbali.

Kifaa hicho huvalishwa katika mkono wa mtoto na hutoa taarifa kuhusu joto.

Joto linapoongezeka, kifaa hicho humfahamisha mzazi kwa kutoa mlio au kutuma taarifa kwenye simu.

Kifaa hicho kinaweza kutumika kwa saa 24 bila kuhitaji kuchajiwa.

Kutumia simu

Kwa kutumia kifaa hiki, wazazi wanaweza kufuatilia hali ya mtoto kupitia simu bila kumsumbua kwa kumgusa mara kwa mara anapolala.

Madaktari wanashauri kuwa mtoto anapopatwa na joto, hufai kumvalisha nguo nzito.

Badala yake mvalishe nguo nyepesi na umpe maji au juisi ya matunda.

Kadhalika, unaweza kumwosha kwa maji vuguvugu.